Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

CHANDE APONGEZA TEKNOLOJIA YA UFUGAJI SAMAKI

Imewekwa: 06 August, 2026
CHANDE APONGEZA TEKNOLOJIA YA UFUGAJI SAMAKI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ufugaji wa samaki baada ya kutembelea mabwawa ya kufugia samaki yaliyopo katika banda la Wizara kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma Agosti 6, 2026.

Akizungumza baada ya kutembelea mabwawa hayo Mhe. Chande alisema teknolojia inayotumika katika ufugaji wa samaki inaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya uvuvi kupitia matumizi ya mbinu za kisasa zinazoongeza uzalishaji kuboresha usalama wa chakula na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Chande aliwataka wananchi hususan vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya ufugaji wa samaki kwa kujifunza teknolojia hizo na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji wa samaki hatua ambayo itasaidia kuongeza ajira, kipato na upatikanaji wa lishe bora.

Sambamba na hilo Mhe. Chande alitembelea banda la Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, ambapo alifurahishwa na namna idara hiyo inavyotoa elimu kwa vitendo kwa wananchi kupitia maonesho ya mashine ya kuchakata malisho pamoja na aina mbalimbali za malisho zilizopandwa katika eneo la maonesho. 

Vilevile alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wafugaji kuhusu matumizi ya teknolojia na mbinu bora za uzalishaji wa malisho yenye tija kwa maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo