ZIWA IKIMBA KUVUNA TANI 13 ZA SAMAKI BAADA YA MIEZI 6

Imewekwa: Thursday 13, March 2025

ZIWA IKIMBA KUVUNA TANI 13 ZA SAMAKI BAADA YA MIEZI 6

◼️ Ni baada ya kupandwa Vifaranga Mil.1.5 vya samaki vilivyofanyiwa utafiti kwenye ziwa hilo

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa zoezi la upandaji vifaranga vya samaki Mil.1.5 kwenye Ziwa Ikimba lililopo mkoani Kagera litaongeza mavuno ya samaki kwa mwaka kwenye ziwa hilo kutoka Tani 1 inayovunwa hivi sasa hadi tani 13 baada ya miezi 6.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa upandaji wa vifaranga hivyo na kukabidhi boti moja ya doria Machi 12, 2025 kwenye mwalo wa Buterankuzi ambapo amewataka wananchi wa kata zote zinazonufaika na ziwa hilo kulinda vifaranga hivyo ili waweze kunufaika na mavuno kwenye ziwa hilo.

"Lakini pia naelekeza wataalam wangu kabla hamjaondoa, mfanye tathmini kama ndani ya Ziwa Ikimba kunaweza kufanyika ufugaji wa vizimba ili wananchi hawa wanufaike zaidi na uwepo wa ziwa hili" Amesema Mhe. Dkt. Kijaji

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji ametumia fursa hiyo kutangaza upumzishwaji wa ziwa hilo kwa miezi 6 ili kuvipa nafasi vifaranga hivyo kukua hadi kufikia hatua ya matumizi kibiashara huku pia akitangaza kufanyika kwa doria ya wakati wote kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali zilizopo kwenye ziwa hilo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kaibanja ambayo ni miongoni mwa kata zinazohudumiwa na ziwa hilo Mhe. Jackson Rwankomezi amesema kuwa hali ya upatikanaji wa samaki katika ziwa hilo kwa sasa haikidhi hata mahitaji ya chakula hivyo wananchi wameamua kwa hiyari zoezi hilo ili waweze kunufaika kijamii na kukuza uchumi wao.

.