ZAO LA MWANI KUINGIZWA KWENYE MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia idara ya ukuzaji viumbe maji kwa kushirikiana na bodi ya usimamizi wa stakabadhi za ghala imeanza mazungumzo ya kuja na mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la mwani ili kuimarisha bei ya zao hilo kwa kuwa na uhakika wa soko na kuwaondolea wananchi unyonyaji kutoka kwa madalali.
Hatua hiyo imejiri mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Bw. Bangu Asangye na Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Nazael Madalla, kujadili maandalizi ya kuanzisha mfumo wa stakabadhi gharani kwa zao la mwani.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Septemba 17, 2025, yakilenga mfumo huo kufanya kazi katika Wilaya za Pangani, Mkinga na Tanga ambayo ni maeneo muhimu katika uzalishaji wa mwani na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Mfumo wa stakabadhi ghalani unatarajiwa kuimarisha bei ya mwani, uhakika wa soko na kuondoa unyonyaji wa madalali.
Mbali na mazungumzo hayo pia, Dkt. Burian, ametoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuwajengea uwezo wavuvi wa mkoa wa Tanga kupitia miradi ya kiuchumi kama ufugaji wa samaki kwenye vizimba ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao