WIZARA ZA KILIMO MIFUGO NA UVUVI ZAANZA NA MAMBO MANNE YA MASHIRIKIANO
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeanza kutekeleza mkakati wa kuimarisha ushirikiano baina ya sekta hizo kwa lengo la kutatua changamoto zinazochangia migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kuongeza tija katika uzalishaji.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, kufanya ziara leo, Septemba 11, 2026, katika Skimu ya Umwagiliaji ya Bonde la Mkombozi na Mradi wa Visima kwa ajili ya wafugaji katika eneo la Mboliboli, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa.
Akizungumza na wakulima na wafugaji baada ya kukagua miradi hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametaja mambo manne ya msingi yatakayozingatiwa katika ushirikiano kati ya Wizara hizo.
Mambo hayo ni kujenga mahusiano mema ya wazalishaji wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili kukomesha uhasama na ugomvi baina ya wafugaji na wakulima, eneo la pili ni kutumia mabwawa ya umwagiliaji kufugia samaki, kushirikishana katika miradi ya vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) na kuwa na mahusiano na mashirikiano ya kimataifa kati wizara hizo mbili huku msisitizo wake akiwataka wafugaji na wakulima kuata sheria na kuwa na matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema katika utekelezaji wa Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Bonde la Mkombozi unaogharimu Shilingi bilioni 76, Wizara yake kupitia Tume ya Umwagiliaji itafunga mfumo wa sola na mitambo ya kusambaza maji katika kisimba cha wafugaji kilichopo Mboliboli.
Aidha, Mhe. Chongolo ameitaka Tume ya Umwagiliaji ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuchimba visima vingine vitatu katika eneo hilo, ili kufikisha jumla ya visima vinne kwa ajili ya kuwahudumia wafugaji.
Mhe. Chongolo pia amewataka wananchi, wakiwemo wakulima na wafugaji nchini, kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatunza chakula cha kutosha kwa matumizi ya baadaye.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Benjamin Sitta amelipongeza jeshi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yanayokaliwa na wakulima na wafugaji, hatua ambayo imechangia kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo hayo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mhe. Emanuela Kaganda, amesema kukamilika kwa Skimu ya Umwagiliaji ya Bonde la Mkombozi pamoja na visimba vya maji eneo la Mboliboli kutawawezesha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji kwa tija zaidi, huku baadhi ya wananchi wamepongeza jitihada zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutatua changamoto zinazosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ingawa upatikanaji wa maeneo ya malisho bado ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele.