KAMANI AWEKA BAYANA UBORA NA USALAMA WA SAMAKI WA KUFUGWA
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amesema Samaki wanaofugwa kwa njia ya vizimba na mabwawa hawana changamoto yeyote na ni salama na bora kwa matumizi ya chakula.
Mhe. Kamani ameyasema hayo leo, Septemba 13, 2026, Wilayani Sengerema jijini Mwanza, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani hapo alipomtembelea muwekezaji wa Sekta ya Uvuvi Kampuni ya Ukuzaji Viumbemaji ya Tanzania Zhongzhi Aquaculture Company Limited.
Aidha, Mhe. Kamani amesisitiza kuwa chakula kinachotumika kulishia Samaki ufanyiwa uhakiki wa mara kwa mara ili kuzingatia ubora unaohitajika na Wizara.
"Samaki hawa wanapimwa kisayansi katika Maabara ya Taifa ya Uvuvi, na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) wanafanya utafiti wa ubora wa Vifaranga vya Samaki na kufuatilia ubora wa mazingira ya samaki wanapofugwa" amesema Mhe. Kamani
Aidha, Mhe. Kamani amewataka vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa za mikopo ambayo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo mikopo ya Boti, Vizimba na Mifugo, ambapo vijana wanawezeshwa kuanzia kupata vifaranga vya Samaki, kuku, ng'ombe na vifaa vingine pamoja na miundombinu mbalimbali.
Vilevile, Mhe. Kamani amesema serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Tasnia ya Ukuzaji Viumbemaji maji ili kuongeza uzalishaji wenye tija na kutengeneza ajira kwa vijana ili kuwaongezea vipato, na amewataka vijana wa Kitanzania kujifunza ujuzi wa utumizi wa teknolojia za kisasa za ufugaji Samaki kutoka kwa wawekezaji ili kuongeza tija katika shughuli zao za uzalishaji na ukuzaji viumbemaji.