UWAZIRI WANGU HAUNA MAANA KAMA HAUBADILI MAISHA YA WAFUGAJI-DKT. BASHIRU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa kiapo alichokula wakati akiteuliwa kushika wadhifa huo kinamtaka kusimamia maslahi ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kwenye ufukara na kudhibiti matapeli wanaodhulumu wafugaji.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo wakati wa kikao chake kilicholenga kutathmini hali ya utendaji na kutafuta suluhu ya kukinusuru kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga Fresh kilichofanyika Februari 18,2026 jijini Tanga.
“Uwaziri wangu hauna maana kama maziwa ya wafugaji yanamwagwa, Uwaziri wangu hauna maana kama wafugaji ni mafukara, Uwaziri wangu hauna maana kama matapeli wanadhulumu wafugaji” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Balozi Dkt. Bashiru amebainisha kuwa kiapo chake kinamlazimisha kusimamia sekta ya Mifugo ili iendeshwe kwa tija, kibiashara, kwa ufanisi na kwa maslahi ya wafugaji na Taifa.
Akielezea maazimio yaliyotokana na kikao hicho, Balozi Dkt. Bashiru pamoja na mambo mengine ameelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa kiuchunguzi kwa kipindi cha miezi 2 kuanzia Machi 1,2026 ili kubaini namna matumizi ya fedha za kiwanda hicho yalivyokuwa yakifanyika.
Awali akizungumza wakati wa kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Tanga Fresh Balozi Adadi Rajab amesema kuwa sababu za kuporomoka kwa utendaji wa kiwanda hicho ni kujiondoa kwa mwekezaji ambaye alifanya hivyo kutokana na kutopata faida aliyoitarajia.
“Mwekezaji huyu alijitoa kwa sababu ya uongozi wa kiwanda uliokuwepo ambao ulikuwa ni wa kifahari ambapo walikuwa wakijilipa mishahara mikubwa kuliko mapato yaliyokuwa yakitokana na mauzo ya bidhaa za kiwanda hicho” Ameongeza Balozi Adadi.
Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya amesema kuwa kiwanda hicho ni mkombozi wa kiuchumi kwa upande wa wafugaji wa mkoa wa Tanga na mikoa inayopakana nayo hivyo kuyumba kwake kutasababisha athari kwa watu wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa ufugaji mkoani humo.
Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Chama cha Maendeleo ya Ushirika mkoani Tanga (TDCU) ambapo jukumu la chama hicho huwa ni kukusanya maziwa kutoka kwenye vikundi vinavyokiunda na kupeleka kiwandani na wanachama kunufaika kupitia fedha zinazotokana na bei elekezi ambazo hupatiwa kila ifikapo katikati ya mwezi husika.