ULEGA ASHIRIKI KILELE CHA MKUTANO WA UVUVI MDOGO JIJINI ROMA, ITALIA

Imewekwa: Monday 08, July 2024

ULEGA ASHIRIKI KILELE CHA MKUTANO WA UVUVI MDOGO JIJINI ROMA, ITALIA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega yupo nchini Italia kushiriki kilele cha Mkutano wa Uvuvi Mdogo Duniani.

Wakati akihutubia mkutano huo Julai 7, 2024 amesema Tanzania ni kinara katika utekelezaji wa Mwongozo wa Kimataifa wa Kusimamia Uvuvi Mdogo, huku akizishajiisha nchi nyingine kuweka dhamira ya dhati katika kutekeleza mwongozo huo.

Alibainisha kuwa nchini Tanzania, asilimia 98 ya shughuli za uvuvi zinafanywa na wavuvi wadogo, na ndio maana serikali kwa kutambua hilo imewatengenezea mifumo mizuri ya kuwakopesha mitaji, ikiwemo kuwapatia vitendea kazi kama vile boti, nyavu, vizimba na vifaa mbalimbali vya kuchakata mazao ya uvuvi na kupunguza upotevu.

Wakati akihutubia mkutano huo, Ulega alieleza kwamba, mwezi uliopita Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa Uvuvi Mdogo barani Afrika, uliohudhuriwa na nchi zaidi ya 33 kutoka Afrika, ambapo kwa pamoja waliweza kupaza sauti za wavuvi wadogo na kuibuka na maazimio ambayo yamewasilishwa na kujumuishwa katika mkutano huo.

Aidha, maazimio ya mkutano huo unaoendelea yatawasilishwa katika Kikao cha Kimataifa cha 36 cha Kamati ya Uvuvi kitachowakutanisha viongozi wa Serikali na wadau kutoka nchi wanachama wa FAO Duniani, kujadili maendeleo, kupanga mikakati na sera za Uvuvi duniani ambacho kinaanza Julai 8-12, 2024.

.