PROF. SHEMDOE AITAKA FETA KUZALISHA WANAOJIAJIRI NA KUAJIRI WENGINE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) kuandaa wahitimu watakaoweza kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiri kuajiriwa kama ilivyo hivi sasa.
Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kilichokutanisha wadau kujadili rasimu ya mitaala 5 inayohuishwa na mitaala 12 mipya iliyoandaliwa na Wakala hiyo 26 Mei, 2025 Mkoani Morogoro.
“Ni lazima tubadilike katika utoaji wetu wa elimu ili kuzingatia mafunzo yanayojikita kwenye ujuzi wa vitendo zaidi ili wahitimu wetu waweze kujiajiri na baadae waajiri wengine” Amesema Prof. Shemdoe.
Aidha Prof. Shemdoe ameielekeza Wakala hiyo kutengeneza mitaala itakayozalisha wataalam wanaozingatia mabadiliko ya tabia nchi kwenye utekelezaji wa shughuli za Uvuvi na ukuzaji Viumbe Maji.
“Mitaala hii pia izingatie teknolojia za kisasa ikiwa ni pamoja na matumizi ya zana mpya za Uvuvi, Ukuzaji viumbe Maji lakini mwisho mitaala hii lazima izingatie matumizi ya Akili Mnemba kwa sababu tusipoliangali hili tunaweza kujikuta siku za usoni tunasahihisha kazi iliyofanywa kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo” Ameongeza Prof. Shemdoe.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt, Semvua Mzighani amesema kuwa Mitaala inayotarajiwa kuanzishwa itasaidia kutengeneza wataalamu waliobobea katika sekta ya uvuvi ambao watasaidia katika kukuza uchumi wa buluu.
" Serikali inakamilisha ujenzi wa Bandari za Uvuvi za Kilwa na Bagamoyo hivyo tunataka wataalamu watakaozalishwa kutokana na mitaaala hii mipya waende kusaidia katika usimamizi wa Bandari hizi" Ameongeza Dkt Mzighani.
Kikao hicho cha kuhuisha mitaala
ya zamani na kuanzisha mitaala mipya kitafanyika kwa muda wa siku 10 ambapo kimeshirikisha wadau kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Sekretarieti ya Ajira na Shirika lisilo la Serikali la Sustainable Agriculture Tanzania (SAT).