TUMEFANIKIWA UPANDE WA MALISHO YA MIFUGO, UFUGAJI SAMAKI-BALOZI KHAMIS
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Musa Omar amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye eneo la uzalishaji wa malisho ya mifugo na ufugaji wa samaki ukilinganisha na hali ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
Balozi Omar amebainisha hayo Agosti 02,2026 wakati wa ziara yake kwenye Taasisi za Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI), Taasisi ya Mafunzo ya Mifugo (LITA),mashamba ya malisho ya Mifugo na mabwawa ya kufugia samaki yaliyopo eneo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya kitaifa na kimataifa ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijiji Dodoma.
“Kwenye malisho kuna mafanikio makubwa kwa sababu tumekuja na mbegu mpya mfano haya majani ya juncao ambayo asili yake ni China na tumeambiwa hapa unaweza kuzalisha mpaka tani 60 katika ekari moja tu na hii inaweza kuwa ni suluhu kubwa ya changamoto ya wakulima na wafugaji” Amesema Mhe. Balozi Omar.
Akizungumzia upande wa ufugaji wa samaki Mhe. Balozi Omar amesema kuwa eneo hilo limeonekana kuwa na tija hasa ikizingatiwa halichukui eneo kubwa na ni chanzo kingine kikubwa cha kipato kwa wananchi.
“Jambo jingine zuri samaki hawa wanaweza kufugwa popote pale na tumeona mfano mkoa wa Singida ambapo ni katikati ya nchi lakini mtu anaweka miundombinu yake kupitia msaada wa wataalam wetu wanapata mafanikio mazuri kwa hiyo kwa hakika tumepiga hatua kubwa” Amesema Mhe. Balozi Omar.
Ziara hiyo ya Mhe. Omar kwenye mashamba ya sekta za Mifugo na Uvuvi inafuatiwa na ile iliyofanywa Agosti 01,2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.