TANZANIA YA TATU AFRIKA MPANGO RASMI WA KUDHIBITI KICHAA CHA MBWA

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya ya wanyama imeandaa Mpango Rasmi wa kutokomeza Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa ikiwa ni moja ya mkakati wa kufikia azma ya Dunia ya kuondokana kabisa na ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi Agnes Meena katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Kitaifa yaliyofanyika leo Septemba 29, 2025 Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
Bi. Meena amesema kwamba mpango huo ambao umeshapitiwa na kuridhiwa na Shirika la Afya ya Wanyama duniani (WOAH) utaratibu wa uchanji wa mbwa na paka wote nchini kwa muda wa miaka mitano.
“Kupitia mpango huo, ni imani yetu kwamba hadi kufikia mwaka 2030 Tanzania itakua ni miongoni mwa nchi zitakazokuwa zimeutokomeza ugonjwa huu wa Kichaa cha Mbwa”,amesema Bi Meena.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa wataalam wa mifugo walio karibu yao au serikali ya mtaa ya eneo husika endapo watakutana na mnyama au mfugo wenye dalili zisizo za kawaida.
Vilevile amesema kuwa mbwa, paka na wanyama wengine wakitunzwa vizuri wana umuhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu huku akiongeza wasipopewa chanjo ya magonjwa hususani kichaa cha mbwa wanyama hao wanageuka kuwa hatari kwa binadamu.
“Kwa hiyo lengo la maadhimisho haya ambayo yamesababisha tukusanyike hapa leo ni kukumbushana na kuelimishana zaidi jinsi ya kukabiliana na janga hili la ugonjwa wa kichaa cha mbwa”, amesema Bi Meena.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Wanyama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Benezeth Lutege amebainisha kuwa takwimu zinaonesha mpaka kufikia Septemba 29, 2025 wilayani humo wametoa chanjo kwa Mbwa 3653, Paka 212, Kuhasi Mbwa 96, Paka 5 na Kufunga Vizazi Mbwa 52, Paka 26.
Akisoma taarifa ya Wilaya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Bi. Mufandii Msaghaa amesema kwamba wilaya ya Kiteto imejitahidi kuzitekelza sera za serikali kuhusu mifugo hususani kuthibiti magonjwa ya wanyama.
“Serikali imejitahidi kuthibiti magonjwa kwa kutoa kinga ya magonjwa ya wanyama. Kila mwaka wataalam wetu wamekua wakitoa huduma ya chanjo kama sera zinavyotutaka”, amesema Bi. Msaghaa.
Maadhisho ya Ugonjwa wa kichaa mwaka 2025 yamebebwa na kaulimbiu isemayo Kichaa cha Mbwa; “Chukua Hatua Sasa, Mimi, Wewe na Jamii.”