SERIKALI YAKANUSHA KUAGIZA VIFARANGA VYA KUKU KUTOKA NJE
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekanusha taarifa zilizokuwa zimesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa ina mpango wa kuagiza vifaranga vya kuku kutoka nje ya nchi.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa Desemba 24,2025 wakati wa mkutano wa wadau wa sekta za Mifugo na Uvuvi uliofanyika jijini Mwanza.
“Kuna taarifa zinasambazwa na zinawatisha watu, hakuna mpango wowote wa kuleta vifaranga au chochote kinachohusiana na kuku kutoka nchi yoyote na hiyo ni kinyume cha sheria na sisi tunaendesha nchi kwa mujibu wa sheria hivyo zipuuzeni hizo taarifa na chukueni taarifa yangu mimi ambaye ndio msemaji wa sekta za Mifugo na Uvuvi” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amewataka wafugaji wa kuku kusubiri mkakati uliopangwa na Serikali ambao unalenga kulinda masoko na mitaji yao.