Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU BORA ZA NG'OMBE

Imewekwa: 11 February, 2026
SERIKALI KUONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU BORA ZA NG'OMBE

Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya mifugo nchini, kwa lengo la kuboresha mbari za mifugo, kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe, hatua itakayoongeza ubora wa nyama na wingi wa maziwa bora.

Hayo yameelezwa leo Februari 10, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati akizungumza na watendaji wa wizara hiyo katika kikao cha uwasilishaji wa maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amesema serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa malisho bora kwa njia za kisayansi, ikiwemo kuanzisha na kusimamia mashamba ya malisho ya kisasa pamoja na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kufanya tafiti, uzalishaji wa malisho na mbegu bora za mifugo.

"Tunataka kuwa na maabara ya rufaa ya mifugo kitaifa ambayo ina vifaa, nyenzo na mitambo ya kubaini na kudhibiti magonjwa ya mifugo," amesema Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa

Aidha, Mhe. Balozi Dkt.Kakurwa amewataka wataalamu wa mifugo kuzingatia maadili ya taaluma na kazi zao ili waweze kuwashauri kwa uadilifu na kuwajengea uaminifu wafugaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa NAIC, Dkt. Dafay Bura amesema kituo kinafanya kazi ya kuboresha mbari za mifugo kwa  kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa mbegu za kisasa kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji, ambapo kwa mwaka 2025/2026 jumla ya mbegu 49,000 zilizalishwa na kusambazwa kwa wafugaji.

Vilevile, Dkt. Bura ameongeza kuwa juhudi hizo zinaambatana na kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya mifugo na wadau wengine wa mifugo nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo