SERIKALI KUJENGA VIWANDA VIWILI VYA KUZALISHA CHAKULA CHA SAMAKI
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza Mkakati wa kujenga Viwanda viwili vya chakula cha Samaki ili kuhakikisha chakula hicho kinapatikana kwa wingi na kwa urahisi zaidi, hatua ambayo itatatua changamoto za upatikanaji wa chakula hicho kwa wavuvi.
Akizungumza leo Machi 18, 2026 jijini Mwanza katika Kikao cha kujadili Mwongozo wa hiari wa kusimamia wavuvi wadogo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Kisaka Meena amesema kwa sasa Serikali ina Mpango wa kujenga Viwanda viwili vya kuzalisha chakula cha Samaki, Viwanda ambavyo vitajengwa Kilwa na Mwanza.
"Viwanda hivi vitajengwa kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), na Serikali inategemea viwanda hivi vitakuwa msaada kwa wavuvi na wakuzaji Viumbemaji wote nchini" amesema Bi. Meena
Aidha, Bi. Meena amebainisha kuwa kwa kipindi cha nyuma wavuvi walikuwa wanashida sana na vyakula vya Samaki kiasi cha kupelekea vyakula hivyo kuagizwa kutoka nchi za nje na kuwa vya gharama zaidi, ila ndani ya miaka mitatu Tanzania imejitahidi sana kujenga Viwanda vya kutengeneza vyakula vya Samaki, ambapo kuna Viwanda mbalimbali vya kuzalisha vyakula hivyo, ikiwemo kiwanda cha Kibaha na Mwanza.
Vilevile, Bi. Meena amesema kuwa lengo la kuandaa Mwongozo wa hiari wa kusimamia wavuvi wadogo ni pamoja na kuimarisha wavuvi hao ili kuhakikisha kuwa hakuna upotevu wa Mazao ya Uvuvi kabla ya kumfikia mteja.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Nchini, Dkt. Baraka Sekadende amesema Mwongozo huo wa hiari wa kusimamia Uvuvi mdogo umezingatia Jinsia, hususan katika kuwakomboa Wanawake wavuvi kiuchumi.
Pia, Dkt. Sekadende amebainisha kuwa katika Mwongozo huo, Serikali imefanikiwa katika kuandaa Mtandao wa Wanawake wanaojishugulisha na shughuli za uvuvi kwa kuwapatia Mafunzo mbalimbali yakiwemo ya uchakataji Mazao ya Uvuvi na zana za uvuvi kwa kushirikiana na wadau wengine wa Uvuvi kama FAO.
Naye, Mwakilishi Mkazi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini Tanzania, Ndg. Charles Tulai amesema kuwa katika Masoko mbalimbali ya Mazao ya Samaki nchini, Miundombinu imeboreshwa ambapo wavuvi wana zana mbalimbali za kuzuia upotevu wa Mazao ya Uvuvi ili kuweza kutunza na kuongeza ubora wa Mazao hayo kabla ya kumfikia mlaji.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wanaojishughulisha na Uvuvi Tanzania (TAWFA), Bi. Beatrice Mmbaga ameishukuru Wizara na wadau wote wa Sekta ya Uvuvi ikiwemo FAO katika kusaidia Wanawake wanaojishugulisha na shughuli za uvuvi katika kuwanyanyua kiuchumi kwa kuwapatia zana za kazi pamoja na elimu ya Uvuvi.
Bi. Mmbaga ameiomba Wizara kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi zingine, pamoja na vikundi vya Wanawake wanaojishugulisha na shughuli za uvuvi na kujengewa uwezo pamoja na kupatiwa mitaji.