​SERIKALI KUENDELEA KUHAMASISHA ULAJI WA NYAMA NCHINI.

Imewekwa: Tuesday 28, September 2021

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema bado ulaji wa nyama nchini Tanzania ni mdogo ambapo kwa sasa ulaji ni kilo 15 kwa mtu tofauti na tafiti za shirika la chakula Duniani linaloelekeza kila mtu atumie kilo 50 kwa mwaka.

Akizungumza, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Amosy Zephania katika ziara yake ya kikazi katika shamba la kuku la Irvine wilayani siha Mkoani Kilimanjaro Septemba 21,2021 ambapo alisema kuwa kutokana na hali hiyo serikali inatarajia kuendelea kutoa elimu kwa watanzania kuona umuhimu wa ulaji wa nyama.

“Sensa ya mifugo ya mwaka 2019/2020 inanyesha katika kaya zinazijishughulisha na kilimo na ufugaji Tanzania ni zaidi ya milioni saba, kaya zaidi ya milioni nne sawa na asilimia 55. 3 wanafuga kuku kuanzia 10 na kuendelea, hii inaonyesha jinsi tunavyozungumza kuku tu, nazungumzia maisha ya watanzania kwanzia ngazi ya chini hadi juu, "amesema

Amesema ni wajibu wa Kampuni hiyo kuhamasisha wananchi kujikita katika ufugaji wa kuku hali itakayo peleka ongezeko la ulaji wa nyama kwa watanzania.

" Toeni elimu kwa jamii, jitanganezi, zipo pesa katika kila halmashauri nchi nzima fikeni huko, zungumzeni na wakurugenzi wakopesheni kuku vijana, kinamama, watu wenye ulemavu, uwezo wa kulipa upo, kwa kufanya hivyo tutawafikia watanzania wengi zaidi na ulaji wa nyama utaongezeka, "amesema

Kwa upande wake meneja masoko na uendelezaji wa biashara wa Kampuni hiyo nchini, Jeremia Kilato amesema wanazalisha vifaranga zaidi laki 220 kwa wiki, ingawa wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia zaidi ya laki 290 kwa wiki.

" Tunajivunia uzalishaji wa kisasa na wenye ubora wa kimataifa, lakini kwa sasa tunakabiliwa na changamoto, ni ongezeko kubwa la uhitaji wa vifaranga hasa katika kipindi hichi cha Uviko 19, Kampuni imeweka mikakati ya kuweza kununua mashine mpya itakayoongeza uzalishaji kutoka 220 hadi 290,"amesema.

Amesema, wanatarajia kuendelea kusambaza vifaranga katika Wilaya zote na Mikoa yote ambapo hadi sasa tayari wamesambaza katika mikoa 13.

Kwa upande wake meneja wa kituo cha uwekezaji Kanda ya Kaskazini, Bw. Daudi Riganda amesema mwekezaji huyo yupo kihalali na yupo kwenye hatua za mwisho.

.