Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AZINDUA PROGRAMU YA KUONGEZA MAZIWA NCHINI

Imewekwa: 10 September, 2026
DKT. BASHIRU  AZINDUA PROGRAMU YA KUONGEZA MAZIWA NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amezindua Programu ya iMbeju Kilimo – Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa katika Wilaya ya Kyerwa, Mkoani Kagera, akipongeza CRDB Bank Foundation kwa ubunifu unaolenga kuwawezesha wafugaji wadogo kupata rasilimali za uzalishaji, maarifa, huduma za kifedha, bima na masoko.

Akizungumza leo Septemba 08, 2026, katika uzinduzi huo, Balozi Dkt. Bashiru amesema programu hiyo ni mfano wa uchumi jumuishi unaomuwezesha mfugaji kutumia ng’ombe kama rasilimali ya kuzalisha maziwa, maziwa kuzalisha kipato na kipato kujenga uwekezaji huku akitaka usimamizi mzuri wa mifumo ya uwezeshaji wa wafugaji ikiwemo Bima ya mifugo.

Mhe. Waziri amesema mafanikio ya programu hiyo yatapimwa kwa ongezeko la uzalishaji wa maziwa na kipato cha wafugaji na kutoa angalizo kwa taasisi za benki ikiwemo CRDB Foundation kuhusu usimamizi mzuri wa bima za mifugo ili kuwasaidia wafugaji kuzalisha na kuyafikia malengo ya mradi huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Bi. Esther Tully  Mwambapa, amesema lengo la programu hiyo ni kumuwezesha mfugaji mdogo kutoka katika uzalishaji wa kiwango cha chini kwenda kwenye uzalishaji wenye tija, biashara na kipato endelevu kwa kuwaunganisha na maarifa, teknolojia, mitaji, usimamizi wa vihatarishi na masoko, akisisitiza kuwa uwezeshaji huo  hautaishia kwenye kutoa fedha bali utajenga biashara inayoweza kukua na kustawi.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Zaituni Msofe, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera amesema mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa katika mkoa huo na kuwahimiza viongozi wote wa wilaya kuhakikisha huduma za ugani zinatolewa ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo ambapo katika awamu hii ya imbeju kilimo kopa ng'ombe lipa maziwa, jumla ya ng’ombe 1,077 zinalenga kugawiwa kwa wafugaji katika Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Misenyi, huku marejesho ya mkopo yakifanyika kupitia maziwa yatakayozalishwa.

Sekta ya maziwa nchini imeendelea kukua, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka takribani lita bilioni 3.9 mwaka 2023/2024 hadi lita bilioni 4.2 mwaka 2025/2026, sawa na takribani asilimia 97 ya lengo la kuzalisha lita bilioni 4.3 kwa mwaka.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo