SEKTA YA MIFUGO SMT NA SMZ ZAIMARISHA USHIRIKIANO

Imewekwa: Saturday 04, March 2023

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zaimarisha ushirikiano Ili kutatua changamoto kwenye Sekta ya Mifugo ili kufikia uzalishaji wenye tija wa mifugo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati akifungua kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) kilichofanyika jijini Dodoma Machi 3, 2023.

‘’Tumekuwa tukishirikiana pia kwenye maeneo ya masoko kuona ni namna gani tunaweza tukaimarisha masoko ya bidhaa za mifugo kwa pande zote mbili. Kwa hiyo ushirikiano huu unalenga kuondoa vikwazo ambavyo vinaweza kuifanya biashara ya mifugo isikue kwa haraka ,’’ alisema Dkt. Mhina

Dkt. Mhina alisema sehemu zote za Bara na Zanzibar kuna viwanda vya kuzalisha bidhaa za mifugo ikiwemo nyama, ngozi, maziwa na bidhaa nyingine hivyo ushirikiano huo utasaidia kuimarisha sekta hiyo ya mifugo.

Aliongeza kwa kusema kuwa ushirikiano huo umelenga kutatua changamoto kwenye maeneo mbalimbali hususan changamoto za kikodi kwa kushauri mamlaka husika ziweze kufanya marekebisho ili kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi zaidi kati ya pande zote mbili za muungano.

"Lakini ushirikiano huu pia utatuwezesha kutumia fursa za pamoja kama zitakuwepo ikiwemo fursa za kusafirisha bidhaa za nyama kwenda nje ya nchi ili tuweze kuyafikia masoko hayo kwa kiasi kikubwa,’’ alifafanua Dkt. Mhina.

Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano huo utajikita pia katika maeneo ya utafiti na mafunzo ili waweze kujifunza kila upande ni namna gani sekta zinafanya ili kuzalisha kwa tija mifugo na bidhaa zake.

‘’Pia tutajifunza ni kwa namna gani wafanyabiashara na wafugaji wa sekta binafsi wanawezeshwa kutumia fursa zilizopo kuzalisha kwa tija na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa,’’ alibainisha

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dkt. Omary Ali Amir alisema wanatumia ushirikiano huo kujifunza tafiti mbalimbali na pia kujenga uwezo wa wataalam wao kupitia Tanzania bara kwa maana Tanzania bara wako mbele kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uzalishaji, Masoko, na Utafiti.

‘’Sekta ya mifugo sio ya muungano, lakini ni sekta ambayo inahitaji ushirikiano, mfano wafugaji wanaposafirisha mifugo kutoka eneo moja kwenda jingine kunakuwa na changamoto za kisera ,kisheria hivyo kupitia ushirikiano huu changamoto nyingi tunaweza kuzimaliza kwa ustawi wa pande zote mbili,’’ alisema Dkt. Omary

.