AZMA YA DKT. SAMIA KWENYE SEKTA ZA UZALISHAJI IMETIMIA-DKT KIJAJI
AZMA YA DKT. SAMIA KWENYE SEKTA ZA UZALISHAJI IMETIMIA-DKT KIJAJI
Imewekwa: 12 May, 2025

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo dhana ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia sekta za Uzalishaji.
Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Hosteli ya wasichana na kumbi mbili za mihadhara kwenye Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa Mei 08, 2025 mkoani Dodoma ambapo mbali na kuupongeza uongozi wa Wilaya ya chuo hicho kwa kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa viwango stahiki amefurahishwa na namna wanafunzi wa chuo hicho walivyoandaliwa kuwa wataalam wazuri wa sekta ya Mifugo.
“Ni wazi kabisa yale ambayo nimejifunza kwa wanafunzi wetu kuanzia kwenye shamba lao la ng’ombe, kitotoleshi cha kuku na hatimaye kwenye kuku wenyewe yametosha kuonesha kazi aliyoamua kuifanya Daktari Samia Suluhu Hassan kwenye upande wa sekta za uzalishaji tangu alipoingia madarakani miaka minne iliyopita ambapo aliamini mbali na kuwawezesha vijana kujiajiri, sekta hizi zitasaidia kuinua uchumi wa wananchi wote hasa wale wa kipato cha chini” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa mbali na ujenzi wa majengo hayo na ukarabati wa kampasi mbalimbali za Wakala hiyo zilizogharimu bil.1.9, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu mingine ya Wakala hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa shilingi milioni 168 za ukarabati wa mabweni mawili ya kampasi ya Temeke.
“Aidha kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hii tumeongeza kiwango cha udahili kutoka 3574 mwaka 2021 hadi wanafunzi 4921 mwaka huu na tayari tumepata shilingi bil. 2.05 kwa ajili ya ujenzi wa kumbi 10 za mihadhara katika kampasi za Mabuki, Mpwapwa, Morogoro na Tengeru” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.
Mbali na Ujenzi wa Majengo ya Wakala hiyo yaliyozinduliwa leo ambao umegharimu takribani kiasi cha shilingi bil. 1.6, Wakala hiyo imeanza ujenzi wa Kampasi nyingine mkoani Songwe itakayogharimu shilingi bil. 1.2 hadi kukamilika kwake.