Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

RAIS CHAPO AHIMIZA USHIRIKIANO ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI BAHARI KUU

Imewekwa: 12 May, 2025
RAIS CHAPO AHIMIZA USHIRIKIANO ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI BAHARI KUU
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Fransisco Chapo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana baina ya Tanzania na Msumbiji katika usimamizi wa rasilimali za uvuvi wa bahari kuu ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika tekinolojia za uvuvi. Mhe. Chapo amesema hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) iliyopo Fumba, Zanzibar leo Mei 9, 2025. Katika ziara yake hiyo, Mhe. Chapo alionesha kufurahishwa na muundo wa usimamizi wa uvuvi wa Tanzania hususan kazi inayofanywa na DSFA huku akiahidi kuona uwezakano wa kuanzisha taasisi kama hiyo nchini Msumbiji. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA, Dkt. Emmanuel Sweke, wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Rais Chapo, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya mapato ya Serikali na kuweza kugharamia uendeshaji wa taasisi hiyo, kuimarika ulinzi na usalama wa rasilimali za uvuvi wa bahari kuu. Mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano baina ya DSFA na taasisi nyingine za ndani, za kikanda na kimataifa ikiwemo Kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi (IOTC) na SADC kupitia Kituo chake cha Kuratibu Usimamizi na Ufuatilia wa Uvuvi (MCSCC) kilichopo Msumbiji. Aidha, Dkt. Sweke alitumia fursa hiyo pia kuainisha maeneo ya kipaumbele ya kushirikiana kati ya Tanzania na Msumbiji ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi na rasilimali watu katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi na ujenzi na matumizi ya miundombinu kama bandari za uvuvi akitolea mfano Bandari ya Uvuvi ya Kilwa inayojengwa na Serikali ya Tanzania. Maeneo mengine ni kuwa na msimamo wa pamoja wa kikanda katika kutetea maslahi ya nchi hizi mbili na nchi nyingine jirani ili kufikia malengo ya kukuza uchumi wa sekta ya Uvuvi. Katika ziara yake hiyo, Mhe. Chapo alipokelewa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Shaaban Othman, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Alexander Mnyeti, pamoja na Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wengine kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Mrejesho, Malalamiko au Wazo