PROF. SHEMDOE AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA KAMPUNI YA XI WANG GROUP

Imewekwa: Wednesday 07, February 2024

PROF. SHEMDOE AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA KAMPUNI YA XI WANG GROUP

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amekutana na wawekezaji wa Kampuni ya XI WANG GROUP kutoka nchini China kwa lengo la kujadiliana namna kampuni hiyo inaweza kufanya uwekezaji kwenye sekta ya mifugo hususan uzalishaji wa vyakula vya mifugo hapa nchini.

Prof. Shemdoe amekutana na wawekezaji hao mapema ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo Februari 7, 2024.

Wawekezaji hao walioambatana na Mbunge wa Madaba, Dkt. Joseph Mhagama wametambulisha mradi wao kwa Prof. Shemdoe ambao lengo lake ni kufanya uzalishaji wa mazao ya Soya, Mahindi na Ufuta kwa ajili ya chakula cha mifugo katika shamba la mifugo la Hanga Ngadinda lililopo Halmashauri ya Madaba, mkoani Ruvuma.

Pia, watawawezesha wakulima wadogo kulima mazao hayo kwa wingi kwa ajili ya kutengenezea chakula cha mifugo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe aliwahakikishia ushirikiano wawekezaji hao ili sekta ya mifugo iweze kuwa na mchango mkubwa katika pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Wawekezaji hao ni Bw. Si Ya Feng na Bw. Yan Lei ambao wote ni Wakurugenzi kwenye kampuni hiyo ya XI WANG GROUP.

.