Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

NI JUKUMU LA KILA MTANZANIA KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI-DKT.BASHIRU

Imewekwa: 06 December, 2025
NI JUKUMU LA KILA MTANZANIA KULINDA RASILIMALI ZA UVUVI-DKT.BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally amepiga marufuku matumizi ya maneno “Uvuvi haramu” ambapo badala yake ametaka vitendo hivyo sasa vitambulike kama Uvuvi usiozingatia sheria na watu wanaofanya hivyo watambulike kama wahalifu.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo wakati akizungumza na watendaji na watumishi wa kitengo cha Uhifadhi wa Maeneo Tengefu alipofika kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kitengo hicho Disemba 06,2025 jijini Dar-es-salaam.

“Hakuna Uvuvi haramu, suala la uharamu na uhalali ni suala la Mwenyezi Mungu sasa mtu haramu maana yake aende motoni na sisi hapa duniani na Serikalini hatuna moto wa kupeleka watu wanaovua uvuvi haramu” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kuwa vitendo vya Uvuvi usiozingatia sheria vinatokana na kukosekana kwa utawala wa sheria katika sekta ya Uvuvi suala ambalo amesisitiza kuwa linapaswa kutekelezwa na kila Mtanzania.

“Kwa hiyo mimi sitakuwa na msamiati wa Uvuvi haramu kwa sababu Rais hajateua masheikh, mapadri, wachungaji au mitume bali ameteua Watanzania kusimamia sheria na kama sheria ni dhaifu bunge lipo na mimi ndo ninaiwakilisha sekta ya Uvuvi na Mifugo bungeni kwa hiyo tuimarishe sheria zetu” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa kwa Watanzania popote walipo pindi wanaposhuhudia vitendo vinavyoashiria Uvuvi usiozingatia sheria wahakikishe wanawachukulia hatua za kisheria watu hao.

“We unamuona mtu ana nyavu za kihalifu, anavua kihalifu, wasimamizi wa sheria wanamlinda mhalifu afu wewe mwenye wajibu wa kusimamia utawala wa sheria unalalamika bila kuchukua hatua kwa hiyo hili ni tatizo letu sote na tutakapoanza kudhurika kutokana na uvuvi wa kihalifu tutaumia wote” Amehitimisha Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo