NDAKI: TUTABORESHA SEKTA YA MIFUGO KWA KUJENGA MAJOSHO 129

Imewekwa: Tuesday 30, March 2021

SERIKALI imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 imepanga kuboresha sekta ya mifungo ikiwa ni pamoja na kujenga majosho 129, ili kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, aliyasema hayo jana jijini Dodoma, wakati wizara yake ilipokuwa kiwasilisha bajeti ya sekta ya mifugo kwenye kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo, mifugo na maji.

Alisema, Wizara hiyo imezamilia kufanya maboresho makubwa katika sekta ya mifugo ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo na kuchangia katika pato la taifa.

Ndaki, alisema moja katika eneo ambalo watalifanyia kazi ni kujenga majosho 129, mapya pamoja na kukarabati yaliyopo ili kusaidia wafugaji kupata huduma hizo katika maeneo yao,

“Tutahakikisha kuwa tunajenga majosho kwa ajili ya kuogeshea mifugo kila eneo lenye mifugo nchini lakini pia kukarabati majosho yote yalipo ili kuwezesha wafugaji kupata huduma za ugani katika maeneo yao”alisema

Alisema, pia eneo jingine ambalo watalifanyia kazi ni kuboresha eneo la malisho kwa ajili ya mifugo ili kuwa na malisho ya uhakika na kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

“Katika hili hivi sasa tumepunguza bei ya kukodisha maeneo ya malisho kwa kukodisha kwa Sh. 3,500 kwa heka kwa mfugaji atakaye hitaji eneo la malisho”alisema

Vile vile, alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha wamepanga kukusanya mapato katika sekta kiasi cha Sh. bilioni 50.

Awali akiwasirisha bajeti ya sekta ya mifugo mbele ya katimati hiyo, Katibu Mkuu Wizara mifugo na uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema itasaidia kuongeza thamani ya mifugo.

Alisema, katika mipango ya bajeti ijayo wamepanga kuhakikisha kuwa wanawekeza katika kuboresha afya ya mifugo,pamoja na kutafuta masoko ya mazao ya mifugo.

“Katika kipindi hichi tutahakikisha kuwa tunatafuta masoko katika bidhaa za mazao ya mifugo kama vile nyama, ngozi , maziwa lakini pia kuongeza fursa nyingine ya matumizi ya vitu kama kwato, pembe na manyoya”alisema

Aidha, alisema kuwa tayari wamepata wawekezaji kutoka nchi ya Slovakia, ambao wapenga kuja kuwekeza kiwanda cha kutengeneza mbolea kwa kutumia manyoya, pembe pamoja na kwato.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wafugaji kutumia fursa ya mitamba ya kisasa iliyopo katika Ranchi za taifa kufanya uhimilishaji ili kupata mifugo iliyobora itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuongeza pato la taifa.

.