‚ÄčNDAKI AKUTANA NA WAFANYABIASHARA YA MIFUGO

Imewekwa: Thursday 12, May 2022

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekutana na Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE) kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto wanazokabiliana nazo Wafanyabiashara hao katika shughuli zao za kila siku.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Mei 10, 2022, Wafanyabiashara hao waliwasilisha kero na changamoto mbalimbali kwa Waziri huyo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi utakaosaidia kuwapunguzia madhila wanayopata katika biashara hiyo.

Wakati akiwasilisha taarifa ya Umoja huo, Katibu wa UWAMIMATE, Bw. Elias Mjanja alitaja jumla ya kero 12 ambazo zimekuwa ni kikwazo kwao katika ufanyaji wa biashara hiyo.

Alizitaja kero hizo ni pamoja na utitili wa tozo, leseni za usafirishaji mifugo hai, mifugo isiyo na ubora sokoni, miundombinu chakavu minadani, uwepo wa madalali kwenye minada, kushamili kwa uuzaji wa nyama kiholela.

Kero nyingine ni kodi kubwa kwenye vifaa vya buchani, faini zinazotozwa na Bodi ya Nyama katika ukaguzi bucha, vibali kwa wauzaji wa mifugo minadani, faini kwa wainua mifugo kwenye magari, changamoto ya kituo cha TRA kilichopo Dumila kuhusu mashine za EFD na ushirikiano kati ya Wadau na Wizara.

Akitolea maelekezo kero hizo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema Wizara imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali katika kutatua kero hizo ikiwemo kuanza kukarabati na kujenga minada katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.

Aliongeza kwa kusema Wizara yake itaendelea kushughulikia kero hizo ili biashara ya mifugo na mazao yake iendelee kuwa na tija kwa Wafanyabiashara hao na nchi kwa ujumla.

"Biashara yenu inahusu moja kwa moja Wizara yetu, tunataka mtoke kwenye kulalamika kuhusu kero na changamoto na muende mbali zaidi kimaendeleo na mnufaike", alisema Ndaki

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda aliwasihi Wafanyabiashara hao kuwa pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo waendelee kutii Sheria wakati changamoto hizo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi akiongeza kuwa milango ya Wizara ipo wazi wakati wote wanapopata changamoto wasisite kuwasiliana na Wizara ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo kwa pamoja.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022