Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. NDEMANGA AWATAKA WAVUVI KULINDA NA KUHIFADHI RASILIMALI ZA UVUVI

Imewekwa: 19 November, 2026
MHE. NDEMANGA AWATAKA WAVUVI KULINDA NA KUHIFADHI RASILIMALI ZA UVUVI

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga, amewataka wavuvi na wadau wote wa Sekta ya Uvuvi kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi rasilimali za uvuvi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili ziendelee kuwa chanzo endelevu cha chakula, ajira na kipato kwa wananchi. Ametoa wito huo Novemba 19, 2026, wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani mwaka 2026 yaliyofanyika katika Soko la Samaki Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Ndemanga amesisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa uvuvi na biashara ya mazao ya uvuvi inayofanyika kinyume cha sheria, pamoja na kuimarisha ushiriki wa Jumuiya za Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) na jamii katika kulinda rasilimali hizo, na amesema jukumu la kuhifadhi rasilimali za uvuvi si la Serikali pekee, bali ni la kila mwananchi, hivyo ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Mhe. Ndemanga ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha Sekta ya Uvuvi kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Uvuvi Kilwa Masoko, utoaji wa mikopo ya boti za kisasa, kuendeleza ukuzaji viumbe maji na kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), na ameipongeza Serikali kwa mpango wa kujenga Bandari nyingine ya Kisasa ya Uvuvi Bagamoyo itakayounganishwa na kongani ya viwanda vya kuchakata samaki, akisema uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza ajira, biashara na fursa za kiuchumi, hususan kwa vijana na wanawake.

Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo, “Uwezeshaji Vijana na Wanawake katika Sekta ya Uvuvi kupitia Ajira zenye Staha na Fursa za Kiuchumi, kuelekea Utekelezaji wa DIRA 2050,” Mhe. Ndemanga amewahimiza vijana na wanawake kutumia fursa zilizopo katika uvuvi, ukuzaji viumbe maji, uchakataji, uhifadhi na biashara ya mazao ya uvuvi na amezitaka Halmashauri, viongozi wa Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusimamia rasilimali hizo na kuhakikisha wananchi wananufaika nazo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Afisa Uvuvi Mkuu, Bw. Tumaini Chambua amesema serikali inaendelea kuimarisha Sekta ya Uvuvi, na kwa sasa Sekta hiyo imekuwa kutoka asilimia 2.3 na kufikia asilimia 6.3.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, ambaye ni Afisa Uvuvi, Bw. Kenneth Mrope amesema maadhimisho hayo ni ya Duniani kuote, na wavuvi wana kila sababu kujivunia siku hiyo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo