MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA YAANZA NA WENYE MAHITAJI MAALUM .

Imewekwa: Tuesday 01, June 2021

Bodi ya Maziwa nchini (TDB) imesema katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora imeamua kugawa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum kutokana na virutubisho vilivyopo kwenye maziwa hayo ambavyo vitawasaidia kuimarisha afya zao.

Akizungumza leo (31.05.2021) mara baada ya kuhitimisha siku ya kwanza ya ugawaji maziwa ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na TDB katika maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, kuanzia tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, Afisa Msindikaji wa Maziwa kutoka bodi hiyo Bw. Dotto Nkuba amesema katika siku ya kwanza bodi imetembelea shule tatu za msingi za Mkoa wa Tanga ambazo pia zinawahudumia watoto wenye mahitaji maalum ili kutoa kipaumbele kwa watoto hao kunywa maziwa na kuhamasisha jamii kuwa na utaratibu kwa kunywa maziwa ili kuimarisha afya zao.

“Lengo la kutoa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum tunahimiza kunywa maziwa kutokana na virutubisho vitokanavyo katika maziwa na tumeangalia watoto wa shule kwa siku ya leo na hii haimaanishi watu wengine wasinywe maziwa bali wanywe kwa faida ya afya zao ila hatua hii itakuwa mwendelezo wa kuyafikia makundi mengine.” Amesema Bw. Nkuba

Ameongeza kuwa maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, yanalenga kuhamasisha wananchi kunywa maziwa kwa sababu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote ambavyo ni muhimu kwa mwili wa binadamu hususan maziwa yaliyosindikwa ambayo yamekidhi ubora.

Aidha, amesema Bodi ya Maziwa nchini inahimiza wananchi kunywa maziwa kwa wingi ili kuwa na utamaduni wa kunywa maziwa na kuviwezesha viwanda vya kuchakata maziwa nchini kuuza bidhaa zao kwa wingi.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Tanga Bi. Sakina Mustapha, amesema wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa unywaji maziwa kutokana na maziwa kuwa na madini na vitamini pamoja na maji ambavyo vyote hivyo vinajenga mwili, kulinda mwili, kuongeza ufanisi wa kujenga mifupa sambamba na meno, kupata sukari na nguvu mwilini pamoja na nguvu ya ziada ya kufanya kazi.

Bi. Mustapha amewaasa wananachi kwa ujumla kunywa maziwa walau kikombe kimoja kila siku ili kuuwezesha mwili kuongeza virutubisho muhimu vitokanavyo na maziwa.

Wanafunzi waliopatiwa maziwa leo na Bodi ya Maziwa nchini ni kutoka katika Shule za Msingi Chuda, Nguvumali na Usagara zilizopo jijini Tanga na zoezi la ugawaji litaendelea kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya watu maalum.

Maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanafanyika Mkoani Tanga kuanzia Tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, katika viwanja vya Tangamano yakiwa yamebeba kauli mbiu “Kunywa Maziwa ya Kwetu, Ongeza Uzalishaji na Usindikaji, Kazi Iendelee.”

.