Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

HATUNA DENI NA RAIS SAMIA-WAFUGAJI

Imewekwa: 06 July, 2025
HATUNA DENI NA RAIS SAMIA-WAFUGAJI

Chama cha Wafugaji nchini kupitia Mwenyekiti wao Bw. Murida Mshota kimemshukuru Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya Mifugo na kuwawezesha kufuga kisasa.

Bw. Mshota amesema hayo Julai 04, 2025 Wilayani Bunda wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Mara ambapo amebainisha namna wanavyotarajia kunufaika na fursa ya ruzuku ya chanjo hizo kwa kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji wake.

“Hii chanjo ambayo inatolewa leo  kwa ng’ombe mmoja zamani mfugaji alikuwa akitoa elfu 17 lakini leo Serikali imesema tutoe 500 tu hiyo nyingine wataibeba wenyewe, mbuzi wetu watachanjwa kwa shilingi 300 tu na Kuku watachanjwa bure lakini pia hapa limejengwa josho la kisasa lililogharimu Mil.28 kwa kweli tunasema Asante Dkt. Samia “Ameongeza Bw. Mshota.

Akizungumza na Wafugaji wa mkoa huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali kuendesha zoezi hilo kwa mtindo wa kampeni ya kitaifa tofauti na ilivyokuwa ikifanyika awali ambapo kila mfugaji alikuwa akichanja kwa wakati wake. 

“Mhe. Rais anataka kuona tunaongeza thamani ya mifugo tuliyonayo na anahitaji tuidhihirishie dunia utajiri tulionao kupitia sekta ya Mifugo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa kufanikiwa kwa kampeni hiyo kumetokana na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa wafugaji ambapo amewataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika zoezi hilo litakaloiwezesha Mifugo yao kushindana kwenye soko la kimataifa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mikoa ya Simiyu, Geita, Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo