DKT. BASHIRU AKUTANA NA WATAALAM WA JUNCAO KUTOKA CHINA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, leo Aprili 28, 2026, amekutana na timu ya wataalam kutoka Jamhuri ya Watu wa China na kujadiliana kuhusu utekelezaji wa mradi wa sekta ya mifugo unaohusu uzalishaji wa malisho aina ya Juncao pamoja na uzalishaji wa uyoga.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo imeeleza kuwa mradi huo utahusisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa malisho ya Juncao, uchakataji na uzalishaji wa uyoga wa chakula na tiba, uzalishaji wa mbolea hai (organic fertilizer) kwa kutumia Juncao, pamoja na kuzuia na kudhibiti mmomonyoko wa udongo kwa kutumia malisho hayo.
Mradi wa Juncao unagharimu shilingi bilioni 8.5, ambapo Tanzania Bara itagharimiwa shilingi bilioni 5.4 na Zanzibar shilingi bilioni 3.1. Mradi huu utatekelezwa katika Shamba la Malisho la Serikali Vikuge kwa upande wa Tanzania Bara na Kizimbani kwa Zanzibar, kwa kipindi cha miaka mitatu.