DKT. NCHEMBA AZINDUA MKAKATI WA MIAKA 10 UFUGAJI WA KUKU NCHINI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amezindua mkakati wa miaka 10 wa ufugaji wa kuku ambao umelenga kubadilisha tasnia ya kuku nchini na kuifanya kuwa shindani, jumuishi na endelevu ili kuchangia usalama wa chakula, lishe, ajira, kipato, ukuaji wa uchumi na biashara.
Dkt. Nchemba amezindua mkakati huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonesho ya kitaifa na kimataifa ya NaneNane iliyofanyika Agosti 1,2026 kwenye viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela jijini Dodoma.
“Kuku ni moja ya zao tambulisho kwa mikoa ya kanda ya kati na kaya mbalimbali, na kuzinduliwa kwa Mkakati huu kwa Serikali ni jambo la faraja ambalo litaenda kuleta mageuzi katika Sekta hiyo ndogo ya kuku na kuongeza uzalishaji wenye tija.”amesema Mhe. Dkt. Nchemba.
Aidha Dkt. Nchemba ameielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huo unaleta tija na matokeo chanya kwenye sekta ya ufugaji wa kuku huku akisisitiza ni lazima uwanufaishe wafugaji wakiwemo wa mikoa ya kanda ya kati ambayo kwa muda mrefu imekuwa maarufu kwa ufugaji wa kuku.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa kupitia Mkakati huo Wizara itaendelea kuhamasisha maendeleo ya sekta hiyo ambayo aliongeza kuwa inawanufaisha wananchi wengi hususan wale wenye kipato cha kati na chini.
“Serikali ya awamu ya sita ya Rais chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha uzalishaji na tija kupitia uboreshaji wa mifugo, huduma za afya ya mifugo, udhibiti wa magonjwa, lishe bora ya mifugo, uzalishaji wa malisho, huduma za uhimilishaji, pamoja na kuimarisha masoko na miundombinu ya biashara ya mifugo na mazao yake” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru
Kabla ya uzinduzi wa Mkakati huo Mhe. Dkt. Nchemba alikagua miundombinu ya ufugaji wa samaki kwa njia ya mabwawa na vizimba pamoja eneo la vipando vya malisho ya mifugo na kuonesha kuvutiwa na teknolojia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba vizimba na mabwawa ambapo aliagiza ujuzi huo wa teknolojia ya ufugaji wa samaki kuendelezwa kwa kuwafikia wananchi wengi ili kuongeza tija ya sekta ya uvuvi na usalama wa chakula.