DKT. LUGENDO AITAKA FETA KUZALISHA KWA WINGI NA KUBORESHA BIDHAA ZA MWANI
Mwenyekiti wa Bodi ya Tatu ya Ushauri ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Blandina Lugendo ameitaka FETA kuboresha na kuzalisha zaidi bidhaa za mwani kwa ubora mkubwa na kwa wingi ili kuleta tija katika Sekta ya Uvuvi.
Akizungumza leo Machi 6, 2026 jijini Dodoma katika Kikao cha Kwanza cha Bodi, Dkt. Lugendo amesema soko la mazao ya mwani linapanda kwa kasi sana kwa sababu ni lishe na ni tiba kwa mwanadamu, hivyo ni jumuku la FETA kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa bora za mwani ili watu waweze kuzipata kwa urahisi.
"tunatakiwa kuboresha kwa wingi bidhaa hizi za mwani na tufanye uzalishaji wa kibiashara na wenye tija ambao utaleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla." amesema Dkt. Lugendo
Aidha, Dkt. Lugendo amewataka FETA kuandaa Mpango Mkakati wa Kibiashara wa bidhaa zinazozalishwa na FETA ili kuongeza mapato katika Wakala hiyo.
Vilevile, Dkt. Lugendo ameitaka FETA kutafuta mbinu bora za kulinda viwango vya ubora wa bidhaa zinazozalishwa ili kulinda soko na taswira nzuri ya FETA.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Isa Mzighani amesema kuwa Taasisi itaangalia namna ya kuboresha bidhaa za mwani ili kuleta tija kwenye Sekta ya Uvuvi.
Pia, Dkt. Mzighani amemuhakikishia Mwenyekiti wa Bodi kuwa bidhaa za mwani zitazalishwa kwa wingi na kwa ubora zaidi ili kujenga taswira nzuri ya Taasisi na Serikali.