DKT. BASHIRU AITAKA BBT IWEKEZE KATIKA KUZALISHA MALISHO YA MIFUGO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amezitaka taasisi zinazotekeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kutumia maeneo yao kuzalisha malisho ya mifugo ili kuimarisha ufugaji wa kibiashara.
Ametoa kauli hiyo leo Januari 31, 2026 alipokagua Kituo cha BBT cha unenepeshaji wa mbuzi na kondoo Kongwa mkoani Dodoma, akizitaka Kampuni za Ranchi ya Taifa (NARCO), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa malisho kibiashara, kutokana na kwamba taasisi hizo zina ardhi, utaalam na uzoefu wa kutosha kufanikisha azma hiyo.
“ Vituo vyetu vyote vyenye ardhi kubwa kama hizi TALIRI, NARCO, LITA kwa sababu tunautaalam na uzoefu mkubwa nguvu zote zipelekwe kwenye uzalishaji wa malisho, mimi ningefurahi kuona kuwa hii ni BBT ya malisho” alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amehimiza wafugaji kupewa elimu ya uzalishaji wa malisho na kuagiza utekelezaji wa programu hiyo uishirikishe Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ili kuwafikia vijana wengi zaidi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa BBT kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Dkt. Daudi Mayeji amesema Wizara hiyo imetengewa dola za Marekani milioni 32.8 sawa na shilingi bilioni 81 kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo, huku uwekezaji wa awali wa Kituo cha Kongwa ukiwa dola milioni 11.82.
Programu ya BBT ilianza mwaka 2018 kupitia TALIRI kwa kushirikiana na PASS Trust Tanzania, ikilenga kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia mnyororo wa thamani wa mifugo na kuchangia uchumi wa taifa.