AFYA, LISHE NA MBEGU BORA NI MSINGI WA UZALISHAJI WA MIFUGO NA KUKIDHI MAHITAJI YA MASOKO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewataka wafugaji nchini kuzingatia masuala ya afya, lishe na mbegu bora za mifugo ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha mifugo na mazao yake yanakidhi viwango na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Novemba 20, 2026 jijini Dodoma wakati wa kufungua kikao cha wadau wa mnyororo wa thamani wa nyama kilicholenga kujadili fursa za upatikanaji wa soko la Mauritius, Dkt. Bashiru amesema ubora wa mifugo na mazao yake huanzia katika uwekezaji wa kutosha kwenye lishe, afya na mbegu bora.
Amewataka wafugaji kuhakikisha mifugo inapata malisho bora na ya kutosha, maji safi pamoja na chumvi na virutubisho vinavyohitajika ili kuimarisha afya na ukuaji wake. Amesema hatua hiyo itasaidia kuzalisha mifugo yenye ubora unaokidhi viwango vya soko na kuwawezesha wafugaji kupata fursa za kuuza mifugo yao kwa urahisi na kwa bei nzuri.
Akizungumzia fursa ya soko jipya la wanyama hai nchini Mauritius, Dkt. Bashiru amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, hivyo ni muhimu wadau kutazama zaidi ya kuuza wanyama hai kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa bidhaa na mazao mengine yatokanayo na mifugo, yakiwemo ngozi, manyoya, kwato na pembe.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kusajili mashamba bora ya malisho ili kutambulika na kuwawezesha wafugaji kupata maeneo yenye uhakika wa malisho kwa ajili ya mifugo yao. Vilevile, amehimiza kuwepo kwa mifumo bora ya taarifa za mifugo itakayowezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na kurahisisha shughuli za ufugaji na biashara ya mifugo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kuongeza mauzo ya nyama nje ya nchi hadi kufikia tani 50,000 ifikapo mwaka 2030, kutoka takribani tani 15,000 zinazouzwa kwa sasa, ikilinganishwa na tani 1,000 zilizokuwa zikiuzwa wakati Serikali hiyo ilipoingia madarakani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, ameahidi kutenga maeneo kwa ajili ya ranchi, machinjio, malisho na minada ya mifugo wilayani humo ili kuwawezesha wafugaji kupata maeneo ya uhakika kwa ajili ya ufugaji na uzalishaji wa mifugo yenye ubora. Pia, amewataka wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake kutumia fursa ya soko la Mauritius kukuza biashara zao.
Awali, akimkaribisha Waziri kufungua kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele, amesema kikao hicho kimewakutanisha wafugaji, vyama vya wafugaji, wasindikaji wa mazao ya mifugo, wasafirishaji wa nyama nje ya nchi pamoja na wamiliki wa mashamba ya mifugo kwa lengo la kujadili fursa na maandalizi ya kuingia katika soko la Mauritius.