ZOEZI LA UCHANJAJI MBWA LAENDELEA NZEGA KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA KICHAA CHA MBWA
Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani, Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Septemba 26, 2026 wameendelea na zoezi la utoaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hizo.
Zoezi hilo limefanyika katika maeneo mbalimbali wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yatakayofanyika Septemba 28, katika viwanja vya Mwanhala, Nzega.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Dkt. Christopher Sikombe Kaimu Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa na wadudu, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema zoezi hilo linafanyika katika kata zote za Wilaya ya Nzega kuanzia tarehe 21 Septemba hadi tarehe 28 Septemba ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho hayo.
Dkt. Sikombe amefafanua kuwa chanjo ya kichaa cha mbwa hutolewa mara moja kwa mwaka, na katika wiki hii ya maadhimisho chanjo hiyo inatolewa bure kwa wananchi wote.
Kwa upande wake, Dkt. Sr. Rosamystica Sambu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ametoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa, umuhimu wa kuchanja mbwa na paka ili kuepukana na ugonjwa huo, pamoja na dalili za mbwa mwenye kichaa cha mbwa.
Aidha, Dkt. Sambu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapa chanjo mbwa na paka wao ili kuepukana na madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na mbwa mwenye kichaa cha mbwa, ugonjwa ambao unazuilika kwa asilimia 100 kwa kuchanja.