WIZARA ZA KISEKTA KUSHIRIKIANA KUHUDUMIA WAFUGAJI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kufanya mazungumzo ya awali na Wizara za Kilimo na Maji ili kushirikiana kwenye maeneo ambayo Wizara hizo zinaingiliana kisekta.
Hayo yamebainishwa Januari 08,2026 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani wakati akizungumza na wafugaji kwenye mnada wa Mifugo wa Ndala uliopo Nzega mkoani Tabora.
“Sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeona tukianza kufanya kazi peke yetu hatuwezi kukimbia kwa mwendo mrefu na maelekezo ya Mhe. Rais ni kwamba kwa miaka hii mitano tukimbie kwa mwendo mrefu zaidi hivyo Mhe. Waziri ameshaanza mikakati ya kufanya vikao na Mawaziri wa Kilimo, na Maji” Ameongeza Mhe. Kamani.
Mhe. Kamani ameeleza kuwa kupitia mashirikiano hayo wafugaji wanatarajiwa kupata sehemu za kunyweshea mifugo yao kupitia skimu za umwagiliaji zinazoendeshwa na Wizara ya Kilimo na miradi mikubwa inayotekelezwa na Wizara ya Maji.
Aidha Mhe. Kamani amesisitiza kuwa wakati mabwawa hayo yakiendelea kujengwa kupitia mpango wa muda mrefu,Wizara yake imeshaanza kuandaa utaratibu wa kutekeleza mpango wa muda mfupi wa kuchimba visima virefu vitakavyowasaidia wafugaji wengi kunyweshea mifugo yao.
Akigusia upande wa malisho ya Mifugo, Mhe. Kamani amewataka wafugaji hao kufika kwenye mashamba ya Serikali kununua mbegu zinazopatikana kwa bei ya rukuzu ambapo amewahakikishia ubora na wingi wa malisho yatokanayo na mbegu hizo ukilinganisha na ukubwa wa maeneo watakayoenda kupanda.