WATAALAMU KUTOKA NIGERIA KUJIFUNZA UCHUMI WA BULUU TANZANIA
WATAALAMU KUTOKA NIGERIA KUJIFUNZA UCHUMI WA BULUU TANZANIA
Imewekwa: 21 May, 2025

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Abdul Mhinte, amesema kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza sera ya kukuza Uchumi wa Buluu kwa kutumia rasilimali zake nyingi ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi huo.
Bw. Mhinte ameyasema hayo leo, Mei 20, 2025, alipokuwa akiikaribisha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Riziki Shemdoe, timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Sera na Mipango Kitaifa ya Nigeria (NIPSS), ambayo imewasili nchini kwa ziara ya mafunzo juu ya masuala ya Uchumi wa Buluu.
“Nchi yetu ina rasilimali nyingi zinazochochea maendeleo ya Uchumi wa Buluu, zikiwemo bahari, maziwa na mito, ambazo zimekuwa zikitumika kukuza na kuendeleza sekta hii muhimu,” amesema Bw. Mhinte.
Ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inatoa fursa nyingi, na kusisitiza utayari wa Wizara kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta hiyo kama sehemu ya mpango mpana wa kukuza Uchumi wa Buluu.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu kutoka Nigeria, Bw. Leye Oyebade, ameishukuru Wizara kwa juhudi inazoendelea kuzifanya katika kukuza Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi.
Timu hiyo ya wataalamu kutoka NIPSS imeanza ziara yao nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uchumi wa buluu.