WATAALAM TSAP WAVUTIWA NA UWEKEZAJI TASNIA YA NYAMA

Wataalam kutoka chama cha Wanasayansi ya uzalishaji Mifugo na Uvuvi ( TSAP) wamekoshwa na uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Galaxy kwa upande wa kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya Food kilichopo mkoani Arusha.
Akizungumza mara baada ya kuongoza timu ya wataalam hao kutembelea kiwandani hapo Septemba 25,2025 Katibu wa Chama hicho Prof. George Msalya amesema kuwa uwekezaji uliofanywa kiwandani hapo unaakisi takwimu zilizopo za mauzo ya nyama nje ya nchi ambapo ametoa rai kwa wafugaji kote nchini kuchangamkia fursa ya soko la mifugo yao iliyopo kiwandani hapo.
“Tunafahamu Serikali yetu imepiga hatua kubwa kwa upande wa mauzo ya nyama nje ya nchi na tasnia hii imechangia sana kwenye pato la Taifa” Amesema Prof. Msalya.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda hicho Bw.Daniel Zebene ameishikuru Serikali kwa ushirikiano inaowapatia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata malighafi za kutosha kuchakata kiwandani hapo.
Naye mmoja wa wanachama wa chama hicho aliyefika kiwandani hapo Bi. Jacqueline Nicodemus amesema kuwa ziara hiyo imewapa funzo la namna mfugaji mdogo anavyoweza kunufaika na fursa zilizopo nchini hususan katika tasnia ya nyama.
Mbali na kutembelea kiwanda hicho, timu hiyo ya wataalam pia ilifika katika kiwanda cha kusindika maziwa cha Kilimanjaro ambapo walipata fursa ya kufahamu hatua mbalimbali za usindikaji wa bidhaa hiyo.