WATAALAM 155 WA WANYAMA WAPATIWA USAJILI
Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) limekamilisha mapitio kwa ajili ya kusajili Wataalam wa Wanyama wenye sifa stahiki, pamoja na Vituo mbalimbali vya kutoa Huduma za Afya ya Wanyama, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Sheria ya Veterinari SURA 319.
Akizungumza katika Kikao cha 63 cha Baraza, leo Mei 23 2026 Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka amesema Baraza limepitia na kuridhia kuwapa usajili Wataalam wa Wanyama 155 na Vituo vya Utoaji Huduma za Wanyama 69, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza hilo.
“usajili huu umefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Veterinari SURA 319, pamoja na Kanuni mbalimbali na miongozo ambayo imeangalia uhalali na vigezo mbalimbali stahiki vya Wataalam” amesema Prof. Kusiluka
Aidha, Prof. Kusiluka amewataka Wataalam hao na Vituo hivyo kutoa Huduma hizo kwa kuzungatia Sheria, taratibu, Miongozo na Kanuni zinavyowataka.