WAKUFUNZI 57 KUWA CHACHU YA MAGEUZI UFUGAJI
Wakufunzi 57 wamehitimu mafunzo ya uwezeshaji wa Shamba Darasa la Ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Leo Oktoba 17, 2026, katika Chuo cha Mifugo MATI Uyole, mkoani Mbeya, kwa lengo la kuimarisha ufugaji wenye tija na unaohimili mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), yamewashirikisha wakufunzi kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa.
Akifunga mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mbeya, Bw. Saidi Maditto, amewataka wahitimu kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kuwafikia wafugaji na kutumia ujuzi walioupata kuboresha uzalishaji wa maziwa, kuongeza kipato na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza umuhimu wa kubadili ufugaji kutoka mazoea kwenda kwenye biashara yenye tija.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Chang’a, amewataka washiriki kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao kwa kutekeleza kwa vitendo yote waliyojifunza ili kuchochea mabadiliko kuelekea ufugaji wa kisasa.
Naye Afisa Mwandamizi wa Fedha na Utawala wa Mradi wa C-SDTP, CPA Iddi Kimaro, aliyemwakilisha Mratibu wa Mradi, amesisitiza uwajibikaji, nidhamu, uadilifu na matumizi sahihi ya rasilimali za mradi ili kuhakikisha mafunzo hayo yanaleta matokeo halisi kwa wafugaji.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wakufunzi wenzake, Dkt. Innocent Ngoma amesema mafunzo hayo yaliyohusisha nadharia na vitendo yamewajengea uwezo wa kuwasaidia wafugaji kutatua changamoto zao na kuboresha shughuli za ufugaji.
Kukamilika kwa mafunzo hayo kunatarajiwa kuwezesha uanzishwaji wa mashamba darasa katika halmashauri za mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa, ambako wafugaji watajifunza kwa vitendo kuhusu uboreshaji wa lishe na afya ya ng’ombe wa maziwa, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuinua kipato chao.