Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUMTUNZA MNYAMA PUNDA

Imewekwa: 19 May, 2025
WAFUGAJI WAHIMIZWA KUMTUNZA MNYAMA PUNDA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Abdul Mhinte amesema ni wajibu wa kila mfugaji punda kumtunza mnyama huyo kwani anahaki kama ilivyo kwa wanyama wengine, ikiwemo haki ya kutolala njaa, kutopata maumivu, kupata maji safi na kuwa huru dhidi ya magonjwa na kazi zinazozidi uwezo wake. Bw. Mhinte ameyasema hayo Mei 17, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt Ashatu Kijaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Chambalo, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma. Aidha, Bw. Mhinte aliwasisitiza wafugaji kuhusu umuhimu wa kutambua mchango wa mnyama huyo katika maendeleo ya kiuchumi. “Punda ana haki ya kutopata majeraha au mateso wakati wa kazi, kupata mapumziko ya kutosha na kupewa hifadhi stahiki,” alisema Mhinte, Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Dkt. Benezeth Lutege, amesema biashara ya punda na mazao yake ilisababisha kutoweka kwa wanyama hao barani Afrika hivyo nchi za Afrika zilikubaliana kusitisha biashara hiyo kwa miaka 15. Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania Mbarwa Kivuyo, amebainisha kwamba wamesambaza elimu ya matunzo bora ya punda kwa wafugaji elimu hiyo imejumuisha umuhimu wa lishe bora, upole wakati wa kazi, matumizi ya matandiko ili kuzuia majeraha.
Mrejesho, Malalamiko au Wazo