Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

WAFUGAJI JIFUNZENI KUBORESHA MIFUGO

Imewekwa: 06 July, 2025
WAFUGAJI JIFUNZENI KUBORESHA MIFUGO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena ametoa rai kwa wafugaji wa halmashauri ya Masasi Mji kuongeza tija ya mifugo yao kwa kutumia mbegu bora zitakazowanufaisha kiuchumi ili kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.

Akizungumza na wafugaji wakati wa Uhamazishaji wa kampeni hiyo kwa mkoa wa Mtwara  Bi. Meena amesema wafugaji wanapaswa kujifunza na kutumia mbegu bora za mifugo ili kujiongezea kipato chao  kwa kutumia wafugaji wa ndani walioendelea.

" Kujifunza sio hadi uende nje ya nchi hata hapa ndani kwetu, nendeni mkajifunze kule Kilwa ili na nyie mpate mbegu bora zitakazo wawezesha kuongeza mifugo itakayowaongezea kipato na kuwa matajiri" amesema Bi. Meena.

Kuhusu mpango wa chanjo unaoendelea kutekelezwa nchini Bi. Meena amesema  serikali itafanya ufuatiliaji wa karibu wa Kampeni hiyo nchi nzima ili kutimiza lengo la kudhibiti magonjwa ya mifugo jambo litakalotusaidia kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake katika masoko ya ndani na kimataifa.
" Tunataka kuwafanya wafugaji wetu kuwa matajiri kwahiyo kampeni hii ya Chanjo na Utambuzi kote nchini tutaifuatilia ili tutimize malengo tuliyojiwekea" aliongeza Bi. Meena.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Bahati Geuzye amesema  zaidi ya dozi milioni 1.5 za mdondo wa Kuku, dozi 335,000 za sotoka ya mbuzi na kondoo na dozi 85,000 za homa ya mapafu zitakazo tumika kudhibiti magonjwa ya mifugo.

Bi. Geuzye amewahimiza wataalam na wakurungenzi wa  halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha mpango huo wa chanjo ya mifugo inafanyika kote nchini  ili kuongeza thamani ya mifugo.

Ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena kwa Kanda ya Kusini inahitimisha leo  katika Mkoa wa Ruvuma ambapo amekagua utekelezaji wa kampeni ya chanjo katika mkoa wa Ruvuma.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo