WAFUGAJI HANDENI WAMUAHIDI DKT. SAMIA KUCHANJA MIFUGO KWA WINGI

Wafugaji Wilayani Handeni wameipokea Kampeni ya Chanjo ya Mifugo Kitaifa vizuri na kumuahidi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujitokeza kwa wingi katika kuchanja Mifugo yao ili kutokomeza Magonjwa hayo ya Mifugo ili kuongeza tija kwenye Mifugo.
Akizungumza katika zoezi la Uhamasishaji na Utoaji Chanjo za Mifugo leo Julai 5, 2025 Wilayani Handeni Mkoani Tanga katika Kata ya Mazingara Kijiji cha Suwa, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mazingara, Bw. Rajabu Mwegole, amesema Mifugo inapochanjwa na kutambuliwa inaleta Usalama kwa Mifugo yenyewe na walaji.
“sisi kama Handeni tunashukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kututhamini wafugaji na kutuletea Kampeni hii ya Chanjo za Mifugo Kitaifa, na sisi wafugani tunamuhaidi kuanzia leo hii tunaanza kuchanja Mifugo yetu ili kutokomeza magonjwa ya mifugo na kuongeza tija katika Masoko ya nje ya nchi.” amesema Mhe. Mnzava
Aidha, Bw. Mwegole amewataka Wafugaji wote wa Handeni na Mkoa wa Tanga kiujumla, wajitokeze kwa wingi kuitumia fursa hii ya Mheshimiwa Rais ili kuweka kutokomeza vifo vya Mifugo, kwani bei za chanjo hizi ni sawa na bure kwani chanjo yang'ombe ni tsht. 500, Mbuzi/Kondoo tshs. 300 pamoja na kuku ambao wanachanjwa bure.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba amesema kuwa Mifugo inakabiliwa na Changamoto nyingi ikiwemo changamoto ya maji, Malisho na Magonjwa, na Changamoto ya Magonjwa ndio imekuwa changamoto kubwa sana inayopelekea vifo vya Mifugo na soko la mifugo kuwa duni katika Masoko ya nje.
Vilevile, Prof. Komba amewapa salamu wafugaji kutoka kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kuwa wafugaji waitumie fursa hii adhimu na waikimbilie, kwani chanjo hizi ni salama na zinazalishwa hapa hapa nchini na viwanda vya ndani.
Naye, Mratibu wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa Wilaya ya Handeni na Daktari wa Mifugo wa Wilaya hiyo, Dkt. Key Amiri amesema Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imeshapata Vifaa vyote vya uchanjaji kutoka kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ikiwemo chanjo ya Homa ya Mapafu ya ng'ombe ambayo ni Dozi 100,000, Chanjo ya Ugonjwa wa Sotoka Dozi 240,000 na Chanjo ya tatu Moja kwa ajili ya kuku ambayo inatibu ndui, mafua ya kuku na kideli ambayo ni Dozi 170,000, hereni za Utambuzi na Vifaa vingine.
Halikadhalika, Kaimu Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Wilaya ya Handeni (CCWT), Bw. Clement Soba amesema Serikali ya awamu ya Sita imewatambua wafugaji na hii ni ishara ya kuonyesha kuwa Sekta ya Mifugo ni Sekta muhimu na ndio mana wafugaji wa Handeni wameamua kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuchanja Mifugo kwa lengo na kutokomeza Magonjwa ili kuiwezesha Sekta kukua kiuchumi.
Pia, Bw. Soba amesema wao kama wafugaji wamelipokea zoezi hili na watahakikisha wanashirikiana na Wizara husika katika kutekeleza zoezi hilo kwa kuhamasisha wafugaji wenzao kuchanja Mifugo yao.