WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI UVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA

Serikali Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ukanda wa Ziwa Victoria ni suala linalohitaji ushirikiano wa pamoja baina yake na wadau wote wanaohusika kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi.
Akizungumza wakati wa Kufungua Kikao cha kujadili mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi kwa ukanda wa Ziwa Victoria kilichofanyika Ukumbi wa Nyakahoja jijini Mwanza Agosti 22, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Edwin Mhede alisema wadau wa sekta ya uvuvi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa kwa kuja na mikakati ya pamoja ikiwemo elimu.
“Ni lazima tuungane na kuwa na mikakati ya pamoja kupiga vita vitendo hivi. Sio jukumu la Serikali Kuu pekee; ni wajibu wa kila mdau wa sekta hii wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji, wamiliki wa viwanda vya zana za uvuvi, wauzaji na wasambazaji wa zana za uvuvi pamoja na Serikali za mitaa. Ni ukweli usiopingika kuwa samaki hawa wakitoweka, hakuna hata mmoja atakayesalia katika biashara ya samaki na mazao ya uvuvi” alisema Dkt. Mhede Aliwahimiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi Tanzania Prof. Mohammed Sheikh amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza matumizi ya teknolojia za kulinda rasilimali za Uvuvi ikiwemo mitambo ya kuhifadhi mazao ya uvuvi.
" Kipindi cha masika asilimia 40 ya mazao ya uvuvi hupotea, kwa sasa tumeanza kuja na mitambo ya kisasa ya kuhifadhi mazao ya Uvuvi yasipotee, pia boti za uvuvi tutaziwekea vifuatilizi kwa ajili ya usalama wa maisha ya wavuvi na rasilimali zake", Alisema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Peter Kasele alisema mkoa huo unashirikiana na wataalamu wa Wizara kwa kufanya doria pamoja na kutoa elimu .
Baadhi wa wadau wa sekta ya Uvuvi wakiwemo wavuvi, wachakataji, wasafirishaji, wamiliki viwanda vya zana za uvuvi wamesema udhibiti wa uvuvi haramu utafanikiwa iwapo serikali itasimamia sheria za uvuvi pamoja ulimishaji kufanyika kwa njia ya vyombo vya habari ambapo elimu hiyo ianishe jinsi uvuvi haramu utakavyowaathiri serikali iendelee ujadili mikakati ya pamoja ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya uvuvi katika ukanda wa Ziwa Victoria .
Aidha kwa Mwaka 2024/2025 jumla ya tani 528,750.09 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.42 za mazao y Uvuvi zilivunwa kati ya hizo, tani 486,789.21 zenye thamani ya Shilingi trilioni 3.41 zilivunwa kutoka kwenye Maji ya asili na tani 43, 497.95 zenye thamani ya shilingi bilioni 12.25 zilitokana na ukuzaji viumbe maji.