VIZIMBA VIMEPUNGUZA UHABA WA SAMAKI NCHINI-MNYETI
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Alexander Mnyeti amesema kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba imesaidia nchi kuondokana na changamoto ya upungufu wa samaki nchini.
Mhe. Mnyeti amesema hayo Novemba 20,2026 wakati wa Hafla ya kuwezesha mitaji kwa vijana 85 wanufaika wa programu ya Jenga kesho iliyo bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) watakaofanya shughuli ya kufuga samaki kwa njia ya Vizimba mkoani humo.
“Kama Mhe. Rais asingefanya hivi baada ya muda flani kusingekuwa na samaki wa kula hapa Tanzania kwa sababu maziwa tuliyonayo hayana samaki kwa hivi sasa” Ameongeza Mhe. Mnyeti.
Aidha Mhe. Mnyeti amekemea tabia ya baadhi ya watu kueneza taarifa potofu kuwa samaki wanaofugwa au kuzalishwa kwa njia ya vizimba hawana ubora ukilinganisha na wale wanaopatikana kupitia uvuvi wa asili ambapo amesisitiza kuwa samaki wanaofugwa ni bora kutokana na kujulikana aina ya chakula walichokula.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Bi. Merisia Mparazo amesema kuwa programu hiyo ya BBT-UVUVI ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali kuwezesha vijana kupata ujuzi, mitaji na fursa za ajira kupitia shughuli za uzalishaji katika sekta ya Uvuvi ikiwemo ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba.
“Lengo ni kuwawezesha vijana kujiajiri, kuongeza kipato, kuchangia katika usalama wa chakula na lishe na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla” Amesema Bi. Mparazo.
Tukio la kugawa mitaji kwa wanufaika wa programu ya BBT mkoani Geita limefanyika ikiwa ni siku chache baada ya wanufaika wengine wa awamu hiyo kuanza kuvuna samaki kwenye vizimba walivyopewa Marchi 7,2026 ambapo wamefanikiwa kupata faida ya shilingi Mil. 76.4 kwa samaki waliouzwa kutoka kwenye vizimba 3 pekee.