Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

UNDP NA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI, ZAPANDIKIZA VIFARANGA ELFU 10 ZIWA VICTORIA

Imewekwa: 20 September, 2025
UNDP NA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI, ZAPANDIKIZA VIFARANGA ELFU 10 ZIWA VICTORIA

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi limepandikiza vifaranga vya samaki 10,000 aina ya sato ndani ya Ziwa Victoria ikiwa ni mkakati wa kukuza Uchumi wa Buluu nchini kwa kuzingaria Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Akizungumza (18.09.2025) wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja kufuatilia utendaji kazi katika Sekta ya Uvuvi mkoani Mwanza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede, amesema UNDP imeonesha utayari wa kuungana na serikali katika mpango mkubwa wa kuendeleza Uchumi wa Buluu kwa kuhakikisha unaboreshwa zaidi ambapo shirika hilo limekubali kuendelea kwa mazungumzo zaidi.

Dkt. Mhede ameongeza kuwa, kupandikizwa kwa vifaranga hivyo kwenye vizimba, katika Mwalo wa Shadi, kata ya Luchelele jijini Mwanza ni moja ya mikakati ya kuhakikisha kukuza uwepo wa rasilimali ya samaki ndani ya Ziwa Victoria.

“Tulianza kampeni ya kupandikiza vifaranga vya samaki aina ya sato, jambo hilo limemvutia Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania, hili ni moja ya eneo alilotaka kushuhudia namna linavyofanyika na mwenyewe amepanda na sisi wizara kwa maana ya serikali tumepanda kuonesha kwamba zoezi hili ni endelevu.” amesema Dkt. Mhede

Aidha, ameishukuru Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kwa kutoa vifaranga hivyo, huku akifafanua kuwa miradi yote haiwezi kufanywa na serikali pekee bali inahitaji usaidizi wa aina nyingi ikiwemo mifumo ya maabara, mifumo ya kuzalisha vifaranga pamoja na kufikia hitaji kubwa kwenye kufuga samaki kwa njia ya vizimba na kulilisha Ziwa Victoria lenyewe.

Pia, amesema kunahitajika uwepo wa vifaranga vingi vya samaki pamoja na ubunifu kwa watendaji na watumishi wengine kuwa na rasilimali za pamoja za kuendeleza maeneo ya kando mwa Ziwa Victoria.

Halikadhalika, ametoa wito kwa wananchi wote pamoja na wavuvi kutoingilia maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kukuza na kuhakikisha samaki wanazaliana kwa sababu ni kinyume kisheria na kuwataka wananchi wanaoishi maeneo hayo, kutoa taarifa panapotokea hali kama hiyo ili serikali ifanyie kazi kwa kuchukua hatua za kisheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania Bw. Shigeki Komatsubara, amewaasa wananchi kutumia vyema mazingira ya Ziwa Victoria kwa kuvua samaki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kwamba watakuwa mfano mzuri kwa nchi na wao wenyewe kujipatia faida.

Bw. Komatsubara amefafanua kuwa, katika ziara hiyo imempa changamoto ya kuanza kutafakari namna UNDP inapoweza kuchangia katika maeneo ambayo serikali kwa kushirikiana na wananchi tayari wameanza kuyasimamia katika Sekta ya Uvuvi.

Amesema UNDP itaendelea kufanya mazungumzo na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha maeneo yatakayochochea ukuaji wa Uchumi wa Buluu yanaboreshwa zaidi na kwamba ameweza kujionea na kujifunza maeneo mengi yanayohusu sekta hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Kikundi cha Ulinzi Kishirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) Mwalo wa Shadi, Bw. Laurent Rusato akisoma risala ya kikundi hicho amesema wamepata mafanikio katika kudhibiti uvuvi haramu kwenye mwalo huo.

Aidha, ameiomba UNDP na serikali kuwaongezea nguvu ya kupata vifaa vya kisasa zaidi ili kuendelea kulinda rasilimali za uvuvi na kufanyika kwa uvuvi wenye tija na endelevu.

Katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania Bw. Shigeki Komatsubara, wamefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kukutana na Katibu Tawala wa mkoa huo Bw. Balandya Elikana pamoja na kutembelea Mwalo wa Igombe (Kayenze ndogo) uliopo wilayani Ilemela ili kujionea chanja za kukaushia dagaa za wananchi na kutembelea mtambo wa kukaushia dagaa kwa njia ya jua wa Kampuni ya Millenium Engineers pamoja na eneo la mazalia ya samaki kwenye Ziwa Victoria katika Wilaya ya Nyamagana.

Pia, wametembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) na Maabara ya Taifa ya Uvuvi (NQFL) ili kujionea baadhi ya shughuli wanazofanya katika kukuza Sekta ya Uvuvi kwa kuzingatia viwango vya ubora.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo