TUIFANYE TANZANIA KUWA KITOVU CHA CHAKULA AFRIKA-DKT. MPANGO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha chakula katika ukanda wa Afrika.
Mhe. Dkt. Mpango amesema hayo kupitia hotuba yake ya Ufunguzi wa Maonesho ya kimataifa ya Nane Nane aliyoitoa Agosti 1, 2025 kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesisitiza Viongozi hao kuwa kinara kwenye utekelezaji wa dira ya Taifa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050.
“Pamoja na mambo mengine Viongozi tuna wajibu wa kuwaelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kuweka nguvu zaidi kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni” Amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango amewataka wafugaji kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa wa bidhaa zinazotokana na mifugo ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, kuendeleza uvuvi na ufugaji wa samaki na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwenye miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji wa mazao wa Mifugo na Uvuvi.
Akitoa taarifa ya Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena amesema kuwa katika Maonesho ya hayo ya mwaka huu Wizara yake imejikita katika kuonesha teknolojia za kisasa kwenye uzalishaji wa malisho, ufugaji wa samaki, uzalishaji wa mazao ya Mifugo na uchakataji wa mazao ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuongeza thamani, kupunguza upotevu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Agosti 5 mwaka huu itakuwa ni siku ya Mifugo na Uvuvi katika Maonesho haya ambapo kutakuwa na gwaride la Mifugo na onesho la usimamizi wa rasilimali za Uvuvi kwa kutumia Ndege nyuki lakini pia inaendelea kutoa huduma ya uchanjaji na utambuzi wa Mifugo hapa hapa viwanjani” Ameongeza Bi. Meena.
Mbali na Paredi ya Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Kijiji cha Protini kilichopo viwanjani hapo kwa lengo la kuhamasisha lishe bora itokanayo na mazao ya Mifugo na Uvuvi.