TSAP NI KIELELEZO CHA MAENDELEO SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI NCHINI -BI. MEENA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amesema kuwa Kongamano la kisayansi la chama cha wataalam wa sekta za Mifugo na Uvuvi (TSAP) ni kielelezo cha maendeleo ya sekta hizo.
Bi. Meena amebainisha hayo Septemba 24,2025 jijini Arusha alipokuwa akifungua kongamano la 48 la kisayansi la wataalam hao ambalo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili taarifa za kitafiti zilizofanywa na wataalam hao kwa mwaka mzima na kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hizo.
“Sekta hizi mbili ndo nguzo kuu za uchumi na lishe nchini kwani zina nafasi kubwa katika kuongeza pato la Taifa, ajira na usalama wa nchi” Amesema Bi. Meena.
Aidha Bi. Meena ameongeza kuwa kutokana na muktadha huo kongamano hilo limekuwa jukwaa la kimataifa la kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bunifu za kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wa tija na mwendelezo wa rasilimali za Mifugo na Uvuvi.
“Hivyo wafugaji na wazalishaji wanahimizwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa na vitendea kazi sahihi vitakavyoongeza uzalishaji wenye tija katika sekta za Mifugo na Uvuvi” Amesisitiza Bi. Meena.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa chama hicho cha Wataalam Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa mkutano huo huambatana na malengo makuu manne ambayo ni kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi, kutoa fursa kwa wadau wa sekta hizo kukutana kila mwaka na kubadilishana mawazo, kuboresha ushirikiano wa watalaam wa ndani na nje ya nchi na kushirikiana na vyama vya wataalam wa sekta hizo ndani na nje ya nchi jambo ambalo huibua miradi mbalimbali ya kimataifa inayohusu sekta za Mifugo na Uvuvi.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo kutoka Zanzibar Dkt. Talib Suleiman amesema takribani asilimia 80 ya mifugo inayosindikwa visiwani humo inatoka Tanzania bara hivyo amewataka wafugaji na wataalam wa malisho nchini kutumia fursa ya soko kubwa la mazao hayo lililopo visiwani humo.
Chama cha wanasayansi wa sekta za Mifugo na Uvuvi kilianzishwa mwaka 1973 ambapo wataalam hao hukutana kila mwaka na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta hizo.