TANZANIA YAZINDUA RASMI MRADI WA STOSAR II,KUBORESHA USALAMA NA UBORA WA CHAKULA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), imezindua rasmi Mradi wa STOSAR II unaolenga kuimarisha mifumo ya Sanitary and Phytosanitary (SPS) katika ukanda wa SADC ili kuwezesha biashara salama, ushindani na uendelevu wa mazao ya kilimo na vyakula.
Akizindua mradi huo tarehe 1 Septemba 2025 katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, alisema mradi huo utashughulikia maeneo muhimu yakiwemo afya ya wanyama, afya ya mimea, lishe na maendeleo ya minyororo ya thamani, hususan katika nyanja za uchunguzi na ufuatiliaji wa magonjwa, udhibiti wa ubora, na upatikanaji wa masoko ya kikanda na kimataifa.
“Mkutano huu ni tukio mahususi la kuzindua mradi huu wa kikanda ambao Tanzania ni miongoni mwa wanufaika. Mradi huu unalenga kuimarisha mifumo ya usafi na usalama wa chakula. Ninaposema chakula, simaanishi tu vyakula vya kawaida, bali pia mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kwa kuzingatia afya na usalama wa walaji. Kwa lugha ya kitaalamu, tunasema Sanitary and Phytosanitary Measures (SPS).” alisema Dkt. Mhede.
Akizungumzia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo uliyoanza mwaka 2018, Dkt. Mhede alieleza kuwa zaidi ya wataalamu 150 wa Tanzania tayari wamenufaika kwa kupata mafunzo, ingawa utekelezaji ulikumbwa na changamoto kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 (COVID-19).
“Lengo kuu la awamu ya pili ni kujenga mfumo imara ambapo taarifa za usalama na ubora wa chakula zinapatikana kwa wakati na kuwasilishwa kwa wadau ili kufanya maamuzi sahihi yanayozingatia ushahidi wa kisayansi. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo itaendelea kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio.” aliongeza Dkt. Mhede.
Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Asilia katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania (EU), Bw. Lamine Diallo, alisema Umoja wa Ulaya umekuwa mshirika wa kudumu katika kilimo cha kanda hii kwani kwa miaka mingi wamefanya kazi kwa karibu na Tanzania kupitia programu mbalimbali za kuongeza uzalishaji, kukuza mbinu za kilimo zinazoangalia mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya ya mimea, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na masoko ya kikanda na kimataifa.
“Awamu hii mpya inajenga juu ya mafanikio makubwa ya STOSAR I, ambayo ilikamilika mwaka 2024. Awamu ya kwanza iliweka msingi muhimu kwa kuimarisha mifumo ya taarifa za kilimo, kuongeza uwezo wa kiufundi, na kuboresha usalama wa chakula na lishe katika kanda nzima. Kupitia STOSAR II, maono yetu ya pamoja ni kutoka kwenye hatua ya kuweka misingi hadi kufanikisha matokeo dhahiri, na kutekeleza kikamilifu sera ya kilimo ya kikanda ya SADC ili kutoa manufaa halisi kwa wananchi wa Afrika Mashariki na Kusini.” alisema Bw. Diallo.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa upande wa Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tito Tipo, alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, maendeleo makubwa yametokea katika utekelezaji wa mifumo ya Usafi na Usalama wa Chakula (SPS) nchini Tanzania, licha ya changamoto nyingi ambazo zinaweza kuwa kikwazo katika kuingia kwenye masoko ya kimataifa kama Umoja wa Ulaya (EU), Asia, na masoko mengine.
“Katika kipindi hiki, zaidi ya wakulima 200 wa parachichi wamefanikiwa kuuza mazao yao nje ya nchi, hasa kwenda Afrika Kusini na India. Washirika wa mafunzo pia wamelihakikishia kutokuwepo kwa virusi vya mafua hatari ya ndege (highly pathogenic avian influenza) nchini, pamoja na kutokuwepo kwa ugonjwa wa Fusarium wilt (ugonjwa wa ndizi), jambo ambalo limeimarisha usalama wa mimea. Aidha, kampeni ya chanjo ya Peste des Petits Ruminants (PPR) ilitekelezwa kwa mafanikio, ikiongeza nguvu katika mifumo ya afya ya wanyama. Msingi pia umewekwa ili kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya kuuza nje, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuuza bidhaa kwenda Mauritius.” alisema Dkt. Tipo