TANZANIA YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI KIMATAIFA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amenadi fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania .
Tukio hilo limefanyika wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika katika chumba maalum cha kunadi fursa kijulikanacho kama Deal room Septemba 4, 2025 katika Jiji la Dakar, nchini Senegal.
Bi. Meena ameelezea kuwa Tanzania ina fursa adhimu zinazochochea uwekezaji katika sekta za Mifugo na Uvuvi zikiwemo utajiri wa rasilimali mifugo na uvuvi zinazochangia uhakika wa malighafi viwandani, uwepo wa maji ya asili ya kutosha kama vile bahari, mito, na maziwa ambayo yanawezesha shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji na uwepo wa maeneo kwa ajili ya ufugaji na uzalishaji wa malisho kibiashara.
Vilevile, Bi. Meena alieleza kuwa Tanzania ina soko lililo tayari kwa bidhaa zitakazozalishwa kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu pamoja nafasi ya kijiografia ya nchi inayowezesha kuyafikia kirahisi masoko ya kikanda na kimataifa
Akielezea fursa zilizopo Bi Agnes Meena amebainisha maeneo ya kimkakati ya uwekezaji ambayo ni eneo la Nyama, Maziwa, Kuku, Vyakula vya mifugo na samaki, Ukuzaji wa viumbemaji na uongezaji wa thamani kwa mazao ya mifugo na uvuvi.