Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUTOA MIKOPO KWA WACHUUZI WA SAMAKI

Imewekwa: 28 October, 2026
SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA KUTOA MIKOPO KWA WACHUUZI WA SAMAKI

Serikali inaendelea kuwawezesha watu binafsi na vikundi vya wafanyabiashara wa samaki katika mialo mbalimbali nchini, kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato.

Akijibu swali leo Oktoba 28, 2026 Bungeni Dodoma la Mhe. John Francisco Nzilanyingi, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, aliyetaka kujua umuhimu wa Serikali kukopesha wachuuzi wa samaki katika mialo ya Jiji la Mwanza, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani amesema wafanyabiashara hao ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi, hususan katika ukusanyaji, usafirishaji na uuzaji wa samaki.

Aidha, Mhe. Kamani amesema Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), inatekeleza Programu ya Uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi kupitia Sekta ya Mifugo na Uvuvi, na programu hiyo inalenga kutoa mikopo kwa masharti nafuu kwa watu binafsi, vikundi na kampuni ili kukuza shughuli za biashara na kuongeza fursa za ajira.

Vilevile, Mhe. Kamani ameweka wazi kuwa katika awamu ya kwanza, jumla ya miradi 917 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.86 imewezeshwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo miradi minane ya Jiji la Mwanza yenye thamani ya shilingi milioni 74, na kwa upande wa awamu ya pili, uchambuzi wa maombi 6,875 unaendelea, yakiwemo maombi 79 kutoka Jiji la Mwanza, hatua inayolenga kupanua fursa za mikopo kwa wafanyabiashara wa samaki na wadau wengine wa sekta ya uvuvi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo