Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI YATAKA WADAU KUSHIRIKI KATIKA UHIFADHI NA ULINZI WA BAHARI

Imewekwa: 27 September, 2026
SERIKALI YATAKA WADAU KUSHIRIKI KATIKA UHIFADHI NA ULINZI WA BAHARI

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani amesema Serikali inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ikiwa ni sehemu ya kukuza Uchumi wa Buluu.

Akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya miaka 30 ya Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia na Tamasha la Kisiwa cha Mafia 2026 yaliyofanyika katika Fukwe za Bahari eneo la Utende leo Septemba 26, 2026 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Kamani amesema Serikali inawahimiza Wadau wote na jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutumia rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Uhifadhi wa bahari ni msingi mkuu na nguzo isiyoepukika ya maendeleo endelevu ya Uchumi wa Buluu, kwani rasilimali za kwenye maji, yaani bahari, maziwa na mito, haziwezi kuleta tija ya kiuchumi bila kuhifadhiwa ipasavyo,ilielezwa.

Mhe. Kamani amesema changamoto zikiwemo uvuvi haramu, shughuli zisizofuata taratibu katika maeneo ya hifadhi, mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira, hususan taka za plastiki, zinahitaji ushirikiano wa Serikali, jamii za pwani, wanasayansi, sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo na kuhimiza matumizi ya teknolojia, utafiti na ubunifu katika kuongeza tija kwenye Sekta ya Uvuvi.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo amesema Fursa za bahari zitanufaisha wananchi kwa kufanya uhifadhi wa bahari ambapo wilaya hiyo pia imeshatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na makazi na kueleza kuwa shughuli za utalii wa bahari ambazo ni mazao ya sekta uhufadhi  zimechangia  Shilingi Bilioni 27 mapato ya halmashauri ya Wiyala hiyo.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema mazao ya uvuvi kutoka ndani ya bahari nchini yapo chini ya asilimia 15  ambazo bado ni kidogo ikilinganishwa na malengo yaliyopo, hivyo Serikali itahakikisha inadhibiti uvuvi wa kutumia baruti na uvuvi usiozingatia sheria lakini katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa samaki Wizara itatuma wataalam kufanya utafiti kwa ajili ya kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba baharini.

Naye, Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dkt. Emmanuel Sweke, amesema kuwa uwekezaji unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, sambamba na ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi na matumizi ya rasilimali hizo, ni muhimu katika kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu, huku Bodi ya Wakurungenzi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ikiahidi kutoa ushirikiano, utawala bora katika kutekeleza malengo ya uhifadhi na taasisi hiyo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo