SERIKALI YAKABIDHI MRADI WA SOKO LA SAMAKI LENYE THAMANI YA BIL 1.3 KWA MKANDARASI.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa na mfuko wa maendeleo ya kilimo (IFAD) imekabidhi ujenzi wa soko la samaki katika kata ya kipumbwi, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga wenye thamani ya bil 1.3 kwa Mkandarasi.
Akiongea wakati wa kukabidhi mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi Agness Meena, septemba 17.2025, amesema soko hilo ni matokeo ya dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua kwa tija, inachangia uchumi wa Taifa na pia inaboresha maisha ya wananchi.
Bi. Meena amesema kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi inalenga kufanikisha kuwapatia wavuvi miundombinu ya kisasa ya kupokea, kuhifadhi na kuchakata samaki kwa kuzingatia ubora na usalama wa mazao ya uvuvi, lengo ikiwa ni kupunguza upotevu, kuongeza thamani, kukuza biashara na kuimarisha mapato ya wananchi na serikali kwa ujumla.
"Mradi huu ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya kuboresha sekta ya uvuvi na kuhakikisha inachangia zaidi katika pato la taifa na maisha ya wananchi" Amesema Bi. Meena.
Pia, Bi Meena amesema Wizara kwa kushirikiana na viongozi wa mkoa wa Tanga itasimamia mradi huo kikamilifu kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango ambavyo vimekusudiwa na pia itaendelea kuwekeza katika miradi mingine ya uvuvi Pangani na katika maeneo mbalimbali ya Nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bi. Batilda Burian amesema mradi wa ujenzi wa soko la samaki kipumbwi ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo inaelekeza serikali kuboresha na kujenga miundombinu ya masoko ya mazao ya uvuvi, ili kuongeza tija, thamani na kipato cha wananchi.
"Sote tunafahamu kuwa idadi ya watu wanaojipatia kipato kupitia shughuli za uvuvi nchini imeendelea kuongezeka kutoka watu milioni 4.5 kwa mwaka 2020 hadi zaidi ya milioni 6 kwa mwaka 2025" Amesema Mhe. Burian
Aidha, Mhe. Burian amemsisitiza Mkandarasi wa mradi huo kufanya kazi kwa viwango venye ubora kwa muda uliopangwa na kwa uadilifu wa hali ya juu.
Naye, Mwenyekiti wa chama cha ushirika wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi wa kata ya Kipumbwi Bw. Said Issa ameishukuru serikali kwa kuwaletea soko la dagaa la kimataifa.
Bw. Said Issa amesema soko hilo litakuwa mkombozi kwa wana kipumbwi ambapo bei ambayo wanaipata kwa sasa ni za chini Sana na kwa ujenzi wa soko hilo utasaidia kupata bei nzuri na maslai makubwa kupitia soko litakalojengwa hapo na kuimarika kiuchumi ukilinganisha na walipo sasa hivi.