Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI YAKABIDHI GARI LA UBARIDI KWA CHAMA CHA USHIRIKA WA UVUVI BUKASIGA

Imewekwa: 12 May, 2025
SERIKALI YAKABIDHI  GARI LA UBARIDI  KWA CHAMA CHA USHIRIKA WA UVUVI BUKASIGA
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi gari la ubaridi kwa ajili ya kusafirishia mazao ya uvuvi kwa Chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA Ltd kilichopo Wilaya ya Ukerewe Jijini Mwanza ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa kuboresha usimamizi wa uvuvi, ukuzaji wa viumbe maji, uchumi wa buluu na biashara katika ukanda wa SADC (PROFISHBLUE). Akikabidhi gari hilo kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, leo Aprili 30, 2025 katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amesema serikali inaendelea kuwawezesha wananchi wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi ikiwemo chama cha Ushirika wa uvuvi BUKASIGA ”Serikali imetumia rasilimali zake kuhakikisha BUKASIGA Ltd inasimama, ndio ilisaidiwa na serikali wakati wa kuingia kwenye mchakato shindani wa mradi wa Profishblue ambao unatumia fedha za serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB) mradi unaolenga kuongeza ubora wa mazao na kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi, kwahiyo gari hili likafanye kazi iliyokusudiwa na likasafirishe Samaki tu” amesema Dkt. Mhede. Aidha Dkt. Mhede amemwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Dkt. Baraka Sekadende kukisaidia Chama cha Ushirika wa Uvuvi BUKASIGA kufanya usajili gari hilo pamoja na kuliweka chapa ’branding’ zitakazoonesha usafirishaji wa mazao ya Samaki ili lisitumike kwa matumizi mengine. Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Dkt. Baraka Sekadende akizungumza kwenye hafla hiyo amesema kuanzia mwaka 2019 wizara imefanikiwa kuanzisha vyama vinne vya ushirika wa uvuvi ikiwemo cha BUKASIGA Ltd ambacho ndicho kimekabidhiwa gari hilo litakalopunguza upotevu wa mazao ya uvuvi . Naye Mwakilishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza ambaye ni Mrajisi wa Ushirika mkoani humo Bi. Hilda Boniface ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuvisaidia vyama vya ushirika kukua kupitia sekta ya uvuvi na kutoa wito kwa vyama vyote vya ushirika kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali, huku Mwenyekiti wa chama cha Ushirika BUKASIGA Ltd Bw. Erasto Majura akiishukuru serikali na kuahidi kulisimamia gari hilo liweze kuwanufaisha wanachama na jamii kwa ujumla. Gari ya ubaridi iliyokabidhiwa kwa chama cha ushirika wa Uvuvi cha Bukasiga ina thamani ya dola za kimarekani 87,230.99, pia gali hilo linakadiriwa kuhifadhi samaki kwa muda wa mwaka mmoja ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa PROFISHBLUE unaotekelezwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC
Mrejesho, Malalamiko au Wazo